Apata kazi kwa kusimama na bango barabarani

Kijana wa Kenya Patrick Muthomi ambaye alisimama barabarani na bango kubwa lililosomeka "Naomba kazi" huku akitaja elimu, ufaulu wake na namba yake ya simu hatimaye amepata kazi katika kampuni ya Chandaria Jijini Nairobi..

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye ana shahada ya kwanza ya uhasibu siku chache zilizopita alibuni mbinu mkakati wa kuweza kupata kazi baada ya kuomba kazi katika taasisi binafsi na za umma bila kuambulia kitu ndipo akajitosa katika barabara ya Thika ambapo wasafiri mbalimbali waliweza kushuhudia na wengi kuchukua namba yake.

Akizungumza na EADRIVE ya EAST AFRICA RADIO Patrick amebainisha kwamba baada ya kusimama na bango ameweza kupokea ujumbe mbalimbali zaidi ya 1000 akitakiwa kutuma maombi na kwenda kwenye usaili jambo ambalo hakuafikiana nalo kwa kuwa ameshaenda mara nyingi na kukosa kazi.

“Nimepigiwa simu nyingi kuliko nilivyokuwa nadhani ila wengi walinipongeza na kutaka nitume maombi yangu lakini nilipopigiwa na kampuni ya Chandaria nilienda na baada ya maongezi na usaili wakakubali kuniajiri katika kitengo nilichosomea jambo ambalo limenifanya nijisikie vizuri sana” Amesema Patrick Muthonyi
Ameongeza kuwa amesaini mkataba wa kuanza kazi na kampuni hiyo ambayo alishawahi kuifanyia kazi kwa kutembeza bidhaa mbalimbali ila sasa wamempa mkataba ambao unaanza tarehe 01 Septemba 2016.

“Haikuwa kazi rahisi kusimama barabarani, kuna siku nilikuwa nashinda njaa kabisa lakini nilikuwa na imani kwamba ipo siku nitapata kazi na ndiyo ikatimia, kiukweli nina furaha sana”- Amesema Patrick
Aidha Muthomi amesema vijana ambao wamekata tamaa kama yeye hawatakiwi kulalamika na kukaa nyumbani bali waende ofisi moja baada ya nyingine kwa kuwa vigezo wanavyo na kwamba siku moja Mungu atawaona na kuwafanikisha.