Halmashauri zashauriwa kuchukua madawati mapema


WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Wizarani hapo, kuhusiana na ukamilishwaji wa zabuni ya Madawati waliokuwa wamepewa.

Baadhi ya Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi,alipokuwa akizungumza nao mapema leo Wizarani hapo kuhusiana na ukamilishwaji wa zabuni ya Madawati waliokuwa wamepewa.

Madawati 30,000 mbioni kukamilika ili yaweze kusambazwa katika Mikoa na Halmashauri zote hapa Nchini ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa Serikali wa kutengeneza madawati elfu 60 kwa ajili ya shule za Msingi na Sekondari hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa Leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Akifafanua Dkt. Mwinyi amesema kuwa katika awamu ya pili madawati 20,000 yameshakamilika na yanaweza kuchukuliwa kuanzia sasa kwenda kwenye majimbo yaliyopangiwa kupata madawati hayo.

“Madawati elfu kumi yaliyobaki yatakamilika wakati wowote kabla ya muda wa mwisho uliowekwa”Alisisistiza Dkt. Mwinyi.

Katika kutekeleza mpango huo, awamu yakwanza jumla ya madawati 32,387 yalitengenezwa na yaliyochukuliwa na Wabunge kwa kushirikiana na Halmashauri zao ni 22,721 tu,hivyo madawati 9,666 sawa na asilimia 30% bado hayajachukuliwa na Majimbo husika.

Akitaja Baadhi ya Mikoa iliyonufaika na Madawati hayo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni Tanga madawati 6444, Njombe 3222,Iringa 3709, Mbeya 3759, Songwe 3222, Rukwa 1611, Ruvuma 4833,Visiwa vya Unguja 3200,Pemba 1800.

Akizungumzia Majimbo ambayo hayajachukua madawati yake katika awamu ya kwanza Dkt.Mwinyi amesema ni vyema Viongozi katika Majimbo hayo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wanatakiwa wakachukue madawati hayo kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Majimbo ambayo hayajachukua madawati yake katika awamu ya kwanza yametajwa kuwa ni Kilindi,Pangani,Makambako,Ludewa,Wangingombe naMakete.

Majimbo mengine ni Kyela,Rungwe,Busokelo,Songwe,Kwela,Tunduru,Iringa Mjini,Mbeya Mjini,Mbeya Vijijini na Ileje Nkasi Kaskazini na Nkasi Kusini.

Tarehe 11 April,2016 Serikali ilitoa zabuni kwa JKT kutengeneza madawati 60,000 kwa gharama ya Bilioni 3 ambapo bei ya kila dawati ni sh 50,000/,aidha tarehe 13 Julai 2016 JKT ilikabidhi madawati 32,387.