Mfumo wa tiketi za elektronikiuwanja wa Taifa kuongeza mapato ya Serikali

  Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akitoa maelekezo ya namna ya kutumia mfumo wa tiketi za eletroniki kwa Waziri wa  Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akikagua vifaa vya mfumo huo katika Uwanja wa Taifa leo Jijini Dar es Salaam Agosti 22,2016.

 Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya(katikati) akimuonesha moja ya mashine ya tiketi za kieletroniki Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye katika Uwanja wa Taifa leo Jijini Dar es Salaam Agosti 22,2016.

Eneo lililowekwa mageti kwa ajili ya mashine za mfumo wa tiketi za eletroniki katika Uwanja wa Taifa.

Serikali inatarajia kuongeza mapato katika Uwanja wa Taifa kwa kutumia mfumo wa tiketi za elektroniki ambapo wateja watahitajika kuwa na   kadi za e-wallet pamoja na kufanya malipo kwa njia ya mtandao ili kuingia uwanjani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokua akikagua vifaa vya mfumo huo leo jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Taifa.

Mhe. Nnauye amesema kuwa Mfumo wa elektroniki unatumia umeme na una UPS inayohifadhi umeme kwa masaa matatu hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusiana na mfumo huo kwani unatarajiwa kukidhi huduma kwa wananchi wote watakaotumia uwanja wa taifa katika matukio mbalimbali.

“Ni vema wananchi mkajenga utamaduni wa kuwahi uwanjani wakati wa mechi ili kurahisisha na kutumia kwa makini mfumo wa elektroniki katika uwanja wa taifa unaotarajiwa kakabidhiwa rasmi tarehe 4 Septemba mwaka huu kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo” alisema Mhe. Nnauye

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Pro. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa mfumo huo wa elektroniki katika uwanja wa taifa ni wa kisasa na utawawezesha watu wote kuingia uwanjani ndani ya dakika 180 hivyo kuokoa muda  wakati wa kuingia uwanjani.

Prof.Gabriel amesema kuwa kila mashine itatumia sekunde mbili kumruhusu mteja kuingia uwanjani tofauti na awali ambapo ilimlazimu mteja kupanga foleni kwa kutumia tiketi za kawaida wakati wa kuingia uwanjani.

Aidha Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Michezo Bw. Makoye Nkenyenge amesema kuwa mradi wa mfumo wa elektroniki katika uwanja wa taifa unaendelea vizuri ambapo hadi sasa mashine 20 za mfumo wa elektroniki zimeshawasili na ujenzi wa sehemu ya miundombinu kwa ajili ya mashine hizo umeshakamilika.