Serikali za mitaa wasitishiwa mikopo na Bodi

BODI ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imesitisha utoaji wa mikopo kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na kuzidai halmashauri nchini zaidi ya Sh bilioni sita huku ikielezwa kuwa utaratibu huo utaendelea hadi hali itakapotengamaa kwa halmashauri kurejesha fedha hizo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Ofisi ya Rais- Tamisemi, Kitengo cha Ukaguzi na Ufuatiliaji wa fedha katika mikoa na halmashauri, Denis Bandisa, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga ambapo hoja hiyo ilihusu hatua ya halmashauri hiyo kuchelewesha utekelezaji wa mradi wa Stendi ya Mabasi ya Mhunze mkoani kutokana na ukosefu wa fedha kutoka kwenye bodi hiyo.

Bandija alisema bodi hiyo imefikia uamuzi huo kufuatia deni inalozidai halmashauri kuwa kubwa, hali iliyosababisha upatikanaji wa mikopo kwenye bodi hiyo kuwa mdogo.

“Bodi inazidai halmashauri fedha nyingi sana tumesitisha utoaji mikopo kwa mwezi mmoja hadi hali itakapotengamaa na fedha hizo zitakaporudishwa na halmashauri,” alisema.

Aidha alisema Tamisemi sasa imeunda kikundi kazi kitakachotoa mapendekezo ya namna ya kupata mikopo kwenye bodi hiyo na kurudishwa kwa wakati ili kuondokana na changamoto iliyojitokeza kwa sasa.

Alisema awali haukuwepo mpango maalumu wa urejeshaji mikopo kwenye bodi hiyo, hali iliyosababisha kuibuka kwa changamoto ya uhaba wa fedha kutokana na fedha hizo kutorudishwa kwa wakati.

Akitoa hoja kwenye kamati hiyo, Mbunge wa Mbagala, Issa Mangungu (CCM), aliitaka halmashauri hiyo kueleza sababu za kucheleweshwa kumalizika kwa mradi wa Stendi ya Mabasi ya Mhunze mkoani Kishapu.

Katika majibu yake, Mhandisi wa Mradi huo katika halmashauri hiyo, Samson Pamphili alisema mradi huo ulikuwa wa awamu mbili na kwamba awamu ya kwanza imekamilika, awamu ya pili imekamilika kwa asilimia 90 tu kutokana na ukosefu wa fedha.