Siasa sasa marufuku ndani na nje

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi jana lilipiga hatua nyingine katika kukabiliana na kile linachoeleza kuwa ni kuchochea wananchi kufanya vurugu, baada ya kupiga marufuku mikutano ya ndani ya vyama vya siasa.

Marufuku hiyo imekuja wakati viongozi wa dini wakiwa wameanzisha mchakato wa kukutanisha viongozi wa siasa na Serikali kutafuta maridhiano ili kuiepusha nchi na uwezekano wa kuingia kwenye vurugu.

Wakati huu, Chadema, ambayo ni chama kikuu cha upinzani nchini, inaendelea na maandalizi ya uzinduzi wa kile inachokiita operesheni ya Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) iliyopangwa kufanyika kote nchini kuanzia Septemba Mosi.

Jana, Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijani aliwaambia waandishi wa habari kuwa walikuwa wameruhusu mikutano kwa sababu walidhani ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na mikakati ya uongozi wa ndani.

“Mkutano unaweza ukawa halali lakini inapofika jambo linalozungumziwa linavunja sheria basi, huo mkutano si halali tena. Hivyo basi kwa kuwa mikutano ya ndani inafanyika kwa namna ambayo si halali, Jeshi la Polisi limepiga marufuku mikutano yote ya ndani kuanzia leo (jana),” alisema Marijani.