UVCCM watangaza maandamano nchi nzima

 Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) nao umesema unatarajia kufanya "maandamano ya amani" nchi nzima Agosti 31 kwa ajili ya kueleza utendaji kazi bora wa Rais Dkt. John Magufuli kwa watanzania.

Wakati Jeshi la Polisi nchini likiwa limepiga marufuku maandamano ya nchi nzima yaliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hii leo Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) nao umesema unatarajia kufanya "maandamano ya amani" nchi nzima Agosti 31 kwa ajili ya kueleza utendaji kazi bora wa Rais Dkt. John Magufuli kwa watanzania.

Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamdu Shaka amesema tayari wameshamwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupata kibali cha maandamano hayo na ulinzi huku akiwaeleza wandishi wa habari kuwa kiu yao ni kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya utendaji wa Rais Dk. Magufuli katika kushamirisha dhana ya maendeleo na kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Maandamano hayo yataanzia katika ngazi za wilaya yataanzia kwenye ofisi za UVCCM ngazi ya wilaya na mkoa na kuishia katika ofisi za wakuu wa wilaya na mikoa huku wanachana wa vyama vingine na wapenda maendeleo wakikaribishwa kujiunga na maandamano hayo ya amani.