Zaidi ya wakazi 1000 mkoani Dodoma wapinga zoezi la ugawaji wa viwanja kinyemela.

Zaidi ya wakazi 1000 wa kutoka kata ya kikuyu kusini manispaa ya Dodoma wamepinga zoezi la ugawaji wa viwanja kwa madai ya kufanyika kinyemela na viongozi wa vijiji kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa manispaa bila kuwashirikishwa huku wakijua wazi kuwa eneo hilo lina mgogoro wa umiliki hali inaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwani hawako tayari kuondoka.

Wakazi hao waliounda tume ya watu 40 iliyoandamana hadi ofisi za mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma kwa ajili ya kushughulikia madai ya kupinga eneo hilo kuuzwa wanasema wanashangazwa na hatua hiyo iliyotokana na ujio wa serikali mjini Dodoma huku wahusika wa uuzaji huo wakijua wazi kuwa bado kuna mgogoro wa ardhi kati yao na mamlaka ya ustawishaji makao makuu CDA na bado muafaka haujafikiwa.

Kufuatia madai hayo kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma Mwl Leonard Msigwa anatoa agizo la kusimamishwa kwa zoezi la ugawaji wa viwanja kwenye eneo hilo hadi muafaka wa mgogoro uliopo upatikane huku akisema ofisi yake itafuatilia hatua kwa hatua mpaka haki ipatikane.

Eneo la Kikuyu kusini lina viwanja vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya 2000 ambapo kwa muda mrefu wananchi wake wamekuwa wakizitaka mamlaka husika kupima ili kuondoa migogoro kwa madai kuwa wameishi kwa muda mrefu.