92% ya watu duniani wanaishi kwenye hewa chafuzi

Uchafuzi wa hali ya hewa

Takwimu mpya za shirika la afya duniani (WHO) kuhusu ubora wa hewa, zimethibitisha kwamba asilimia 92% ya watu duniani wanaishi katika maeneo ambapo viwango vya ubora wa hewa ni vidogo kupita kiasi cha ukomo kilichowekwa na shirika hilo.

Kwa mujibu wa shirika hilo takwimu zinatolewa kwa njia ya ramani ambayo inaonesha mahali palipo na hatari ya hewa chafuzi, na kubainisha hatua za msingi za kufuatilia na kukabiliana na hali hiyo.

Takribani vifo milioni 3 kila mwaka vinahusishwa na hewa chafuzi hasa nje ya nyumba, lakini shirika hilo linasema hata ile ya ndani husababisha vifo pia.

Mwaka 2012 inakadiriwa kwamba vifo milioni 6.5 kote duniani vimetokana na hewa chafuzi ndani na nje ya nyumba huku karibu asilimia 90 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi za kipato cha chini na wastani.