Arusha walalamikia ubovu miundombinu ya maji

Wakazi wa mtaa wa Kambi ya Fisi, kata ya Ngarenaro mkoani Arusha wakivuka daraja ambalo kipindi cha mvua halipitiki na kukata mawasiliano.

Katika kuelekea msimu wa mvua baadhi ya wakazi wa mtaa wa Kambi ya Fisi, kata ya Ngarenaro mkoani Arusha wameuomba uongozi wa serikali ya mkoa, kuchukua tahadhari za mapema katika kuandaa njia za mitaro ya maji taka ili kuepukana na adha ya mafuriko.

Wakazi hao wameeleza kuwa wamekuwa wakipata adha kubwa hususani kipindi cha mvua mara baada ya mitaro kutiririsha maji taka katika makazi ya watu jambo ambalo linahatarisha maisha yao.

Wakazi hao walifikisha malalamiko yao ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha ambayo aliagiza mkandarasi kurekebisha miundombinu hiyo katika kipindi cha siku tisini lakini mpaka sasa hakuna kulicho fanyika, hivyo kumuomba mkuu mpya wa mkoa kuingilia kati.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa kambi ya fisi Hillary Mkony amekiri kuwepo kwa tatizo hilo huku akidai kuwa mpaka sasa suala hilo ni kitendawili huku maisha ya wakazi wa mtaa wake yakiwa hatarini.

Mtaa wa kambi ya fisi ni moja kati ya mitaa yenye watu wengi zaidi jijini Arusha,ambapo inaelezwa kuwa ujenzi wake haukufuata ramani ya jiji hivyo kujenga ki holela.