Jaji Warioba: Nchi imepoteza mwelekeo

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema kwa sasa nchi imepoteza mwelekeo katika masuala ya itikadi, Sera na maendeleo, badala yake imebaki kuongozwa kisiasa na matukio.

Akizungumza katika mhadhara wa tatu wa Mwalimu Nyerere leo Dar es salaam, Warioba aliyekuwa Mgeni rasmi amesema tofauti na zamani kulipokuwa na ubaguzi wa makabila, siku hizi watu wanabaguana kwa vyama.

"Sijui kama tuna itikadi na Sera siku hizi, tunategemea matukio na watu" alisema na kuongeza: "Siku hizi wananchi hawajui tunaelekea wapi, zamani kulikuwa na Sera na itikadi, lakini hata ukiangalia vyombo vya habari ni siasa tu." Amesema na kuongeza:

 "Zamani kina Kahama (Sir George) walikuwa wanahamasisha maendeleo,  siku hizi viongozi wetu wanakwenda kushitakiana kwa wananchi."

Mhadhara huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Gharib Bilal, Waziri wa zamani, Sir George Kahama na wasomi mbalimbali.