Makonda: wanaobeza jitihada za Rais Magufuli, ‘hawajui wanalolitaka’

 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemmwagia sifa Rais John Magufuli kwa utendaji wake na kusema yeye ni mtu wa kutenda na sio maneno huku akiwapa vidonge vya wale wanaobeza jitihada zake.

Makonda ametoa kauli hiyo Jumatano hii kwenye uzinduzi wa ndege mpya za ATCL kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Rais naomba uendelee kutenda, sisi tumegawanyika kwenye upande wa fikra,kuna watu ambao hawajui wanachokitaka na hata ukiwafanyie yale ambayo ulifikiriA wao wanayataka kumbe sio,” alisema Makonda.

“Ikumbukwe wakati wa bunge tulikuwa tunafuatilia kusikiliza, Tanzania haina ndege tumezidiwa katika nchi za Rwanda tumezidiwa na wapi, umenunua ndege wanaanza kusema ndege zenyewe hazijang’aa, wamekuja kuzioshea airport, hawajui nini wanachokitaka. Hao hao walipiga kelele tunataka elimu bure,angalau na wananchi wa hali ya chini wapate elimu bure, wameanza kusema elimu yenyewe bure wakati majengo yanadondoka! Kwahiyo hawajui wanalolitaka. Hawa hawa wana lalamika foleni Dar es Salaam, umeamua kutujengea barabara hizo hela za barabara ingeenda kwenye chakula tunakufa na njaa, mheshimiwa rais hawajui wanalolitaka,” alieleza.

“Sisi tunaojua tunalolitaka tupo pamoja na wewe, tunakuunga mkono usiku na mchana na tutaendelea kukuunga mkono usiku na mchana na ninaamini kwamba wanasiasa wengi wanasubiri kutimiza ahadi zao katikati au mwishoni mwa kuelekea kampeni wewe hujasubiri, uliahidi ndege mwaka jana leo hata mwaka hujamaliza ndege zimeingia, wewe ni mtendaji ambaye tutaendelea kukuombea,” alisisitiza.