Meja mstaafu apandishwa kizimbani kwa ujangili

Dar es Salaam. Meja  Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) Salum Athuman Kamota (74) na wenzake watatu  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na Meno ya Tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh 190 milioni na silaha.

Wakili wa Serikali, Elia Athanas  leo amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage kuwa mshtakiwa Kamota kati ya Januari Mosi , 2006 na Septemba 2016 kati ya  mikoa ya Pwani, Tanga na Dar es Salaam alipokea na kusafirisha meno ya Tembo yenye thamani ya Sh 162,750,000.

Athanas alidai kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa Rajabu Mwinyimkuu (42), Jumanne Juma (30) na Said Abdallah (36)  katika  kijiji cha   Ntumbabukang’ondo wote wakazi wa Kisarawe walikutwa wakiwa na vipande vinne vya  meno ya Tembo  yenye thamani ya Sh 32.5 milioni bila ya kuwa na leseni.