Pato la Taifa laongezeka kwa shilingi trilioni 0.8

Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania imetoa taarifa kuhusiana na pato la taifa katika robo ya pili ya mwaka inayoanzia April hadi Juni mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, imeonyesha kuwa pato hilo limepanda na kufikia shilingi trilioni 11.7 kutoka shilingi trilioni 10.9 ilivyokuwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa, ametoa takwimu hizo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa kwa wastani kumekuwa na ongezeko la shughuli za kiuchumi na mapato karibu katika kila sekta.

Hata hivyo Dkt. Chuwa amesema ukuaji wa sekta ya usafirishaji bado unakabiliwa na changamoto ya kushuka kwa biashara ya usafirishaji duniani ambapo ameishauri mamlaka ya bandari kuzunguka nchi za nje kutafuta meli za kuja nchini kwani mpaka sasa zaidi ya meli 700 zimepaki maeneo mbalimbali duniani kwa kukosa shehena ya mizigo kutokana na hali mbaya ya uchumi.