Rais Magufuli aahidi kununua ndege zingine kubwa mbili, ya abiria 160 na 240

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli ameahidi kununuliwa kwa ndege zingine mbili kubwa kwaajili ya shirika la ndege la Tanzania, ATCL.

Ametoa kauli hiyo Jumatano hii kwenye uzinduzi wa ndege mbili mpya za ATCL kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Ndege hizo ni aina ya Bombadier Q 400 zimetengenezwa nchini Canada.

Amesema ndege mbili kubwa zikazonunulia hapo baadaye zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160 na nyingine kubwa zaidi itakayobeba abiria 240 pamoja na mizigo yao. Amewahakikishia Watanzania kuwa fedha za kununua ndege hizo zipo.

Kuhusu ndege mbili zilizotua tayari kwa kuanza kazi, Rais Magufuli amesema serikali ilianza kwa kuzilipia asilimia 40 ya gharama zake na kisha kumalizia asilimia 60 iliyokuwa imesalia na kwamba zingekuwa na gharama zaidi kama zingelipiwa kidogo kidogo.

Rais amedai kuwa ndege hizo zina ubora wa uhakika na zinaweza kufanya kazi katika mazingira yoyote. “Nataka niwahikishie watanzania ndege hizi ni mpya, mzitumie kwa kujua ni mali inayotokana na kodi zenu,” alisema.

Ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria abiria 76, 6 wakiwa daraja la juu na 70 ni daraja la chini.

Pia alitumia fursa hiyo kukanusha madai ya baadhi ya watu kuwa ndege hizo hazikimbii.

“Natamani huyo aliyesema hazina spidi nimjue nimlipie nauli akae mbele aone zinavyokata mawingu,” alitania

Kwa upande mwingine Rais Magufuli amewakumbusha wafanyakazi wa ATCL kufanya kazi kwa weledi na kuepuka kufanya kimazoea huku wakitambua kuwa kuna ushindani katika sekta hiyo. Pia ameagiza wasiruhusu mtu yeyote asipande bure hata kama ni viongozi wa nchi.