Serikali kufanya uhakiki mpya wa watumishi wa umma

Serikali inatarajia kuendesha zoezi la uhakiki wa Watumishi wa umma kote nchini kwa siku 14 kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ili kuondoa watumishi hewa na wenye utambulisho danganyifu.

Akiongea na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaam, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais menejmenti ya utumishi wa umma na utawala bora Mhe. Angellah Kairuki, amesema zoezi hilo litahusisha uchukuaji wa alama za vidole, vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa na hati ya malipo ya mshahara, hati ya kusafiria, kadi ya mpiga kura na Kitambulisho cha Kazi.

Mhe. Kairuki amesema lengo ni kuimarisha mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu na mishahara, kwa kutumia kanzi data ya utambulisho wa Taifa, ambapo zoezi hilo litaendeshwa na mamlaka ya vimbulisho vya taifa, na kwamba zoezi hilo litaanza Oktoba 3,2016.

“Tuna watumishi wa serikali laki 5 na elfu 61, lakini uhakiki huu utatupa fursa ya kuwatambua zaidi watumishi wetu na zoezi hili litahusisha watumishi wote, wakiwepo Polisi lakini upande wa Majeshi (JWTZ) wao wataandaliwa utaratibu wao wakati mwingine” , amesema

Aidha Mhe Kairuki amewataka watumishi kote nchini katika Wizara mbalimbali, Idara za serikali zinazojitegemea, Tawala za Mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, Wakala za Serikali, Taasisi na mashirika ya Umma, ambapo zoezi litahusisha na watumishi wa serikali kwa upende wa Zanzibar.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA Bwana Mohamed Hamisi, amesema tayari wameandaa watumishi 400 kwa ajili ya zoezi hilo kwa nchi nzima, ambapo BVR zaidi ya 5000 zitatumika.