Serikali yaahidi kuboresha taasisi ndogo za fedha

Serikali imeahidi kuendelea kukuza uwezo wa taasisi ndogo ndogo za kifedha nchini kutokana na uwezo wa taasisi hizo katika kuwafikia wajasiriamali wadogo.

Imesema imefikia hatua hiyo hasa kipindi hiki ambapo wajasiriamali hao wamekuwa na umuhimu mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa na malighafi zinazohitajika viwandani.

Kaimu Naibu Kamishna kutoka Wizara ya Fedha Bw. Agustino Olao amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ambapo shirikisho la asasi ndogo ndogo za kifedha nchini TAMFI lilipotoa fedha kwa wajasiriamali wadogo walioonesha nidhamu na matumizi mazuri ya mikopo inayotolewa na taasisi hizo.

Winnie Terry ni Mkurugenzi Mkuu wa TAMFI ambapo akizungumza katika hafla hiyo ameitaja changamoto inayozikabili taasisi ndogo ndogo za kifedha kuwa ni riba kubwa kwa mikopo inayotolewa na taasisi na mabenki makubwa na kwamba hiyo imekuwa ikisababisha riba kubwa kwa mikopo wanayoitoa.