Tanzania yapanda nafasi 4 kwa uwekezaji duniani

Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika eneo la uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji ambapo kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jijini Dar es Salaam leo, Tanzania imepanda kwa nafasi nne ikishika nafasi ya 116 kati ya nchi 138 zilizofanyiwa utafiti.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupunguza Umaskini ya REPOA, Dkt Lucas Katera ndiye aliyetoa ripoti hiyo ambapo ametaja baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri kuwa ni kwenye mifumo ya kifedha, mapambano dhidi ya rushwa, sera na taratibu za kodi pamoja na ukubwa na usimamizi wa soko la bidhaa.

Hata hivyo, Dkt. Katera amesema kama nchi inayoelekea kwenye uchumi wa kati, ripoti hiyo imeonesha kuwa bado juhudi kubwa zinahitajika katika uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano na nishati ili kuvutia idadi kubwa zaidi ya wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini.