Aliyempigisha ‘deki’ Mwalimu aigomea CWT

ELIUD Mwaiteleke, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, aliyeamuru Hamis Sengo, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Shilala kudeki darasa mbele ya wanafunzi ‘amekitolea nje’ Chama Cha Walimu (CWT) mkoani Mwanza baada ya viongozi wake kutaka kumuona na kumtaka aombe radhi, anaandika Moses Mseti.

Tukio la mkurugenzi huyo kumdhalilisha mwalimu huyo mbele ya wanafunzi wake, lilitokea Oktoba 17, mwaka huu shuleni hapo, baada ya ‘bosi’ huyo wa halmashauri kukuta baadhi ya madarasa yakiwa machafu.

Mkurugenzi Mwaiteleke akiwa ameambatana na maofisa wengine wa serikali ngazi ya wilaya hiyo, alifika shuleni hapo majira ya jioni na kumuita mwalimu (Sengo) ili aeleze kwanini madarasa ni machafu na kumtaka kudeki kitendo kilichotekelezwa na mwalimu huyo bila kupinga.

Sibora Kisheri, mwenyekiti wa CWT mkoani hapa amesema kuwa wamelipokea tukio hilo kwa masikitiko na kwamba wamemtaka mkurugenzi huyo kuomba radhi bila mafanikio.

“Tumefanya mazungumzo na tukaazimia kumtaka mkurugenzi huyo kuomba radhi na kumhamisha mwalimu huyo shuleni hapo kwa gharama zake na asifanye kitendo hicho kwa mwalimu mwingine.
Endapo mkurungezi huyo atashindwa kutekeleza maagizo hayo, tutachukua hatua kali zaidi kwani tumechoka kuonewa na viongozi wa serikali kila kukicha.

Kisheri amesema kuwa viongozi wa CWT walienda kuonana na mkurugenzi huyo lakini hakutaka kuonesha ushirikiano kwao na alidai kwamba leo anasafiri hawawezi kuonana na sisi.

“Mkurugenzi ni msimamizi wa watumishi lakini tunashangaa kuona kiongozi kama huyo anageuka kuwa mnyanyasaji na viongozi wasidhani kama sisi ni wanyonge, tunaweza kuchukua maamzi magumu zaidi ya hayo,” amesema Kisheri.

Alipopigiwa simu yake zaidi ya mara tano, ilikuwa ikiita na kukatwa lakini baadae ilipokelewa na mkurugenzi huyo kumtaka mwandishi kuwa yupo barabarani na hawezi kuzungumzia suala hilo.

Mkurugenzi: Nipo barabarani, sikusikii vizuri ni tukio gani?
Mwandishi: Ni tukio la kumuamuru mwalimu kudeki darasa ulilolifanya Oktoba 17.
Mkurugenzi: Ngoja nikutumie namba za afisa habari wa wilaya (Misungwi) atakueleza suala hilo.