BAADA YA TAMKO LA SERIKALI WATUMISHI WAFURIKA VITUO VYA USAJILI

Watumishi wa Umma mkoani Dodoma wamefurika katika vituo vya usajili kufuatia tamko la Serikali la kuongeza muda wa usajili Vitambulisho vya Taifa kufikia Oktoba 31, 2016 ambapo mfanyakazi au mwajiri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hilo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake; tamko lililotolewa na Waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alipokutana na vyombo vya habari hivi karibuni.

Watumishi waliojitokeza katika vituo wameonekana kuwa tayari wamejaza fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa wakiwa wamejipanga kupigwa picha.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amekuwa miongoni mwa viongozi waliotembelea moja wapo ya vituo vya usajili mkoani Dodoma; kushuhudia namna shughuli za usajili zinavyofanyika na kupata taarifa ya mpango wa utekelezaji zoezi hilo ilivyopangwa na mkoa husika, katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati na kila mtumishi anasajiliwa na kuchukuliwa alama za Vidole, saini ya kielektroniki na picha.

Zoezi la Usajili Watumishi wa Umma linaenda sambamba na kuanza kwa uhakiki wa taarifa za uraia wa waombaji wote walioomba kupatiwa Vitambulisho vya Taifa.

Tayari mikoa ambayo usajili umekamilika, zoezi la uhakiki wa taarifa na mapingamizi linaanza mara moja ili vitambulisho kuanza kuzalishwa.