Mwanamke mwingine asema alidhalilishwa na Trump

 Karena Virginia: "Nilijihisi kudhulumiwa na kukosa uwezo"

Mwanamke wa kumi sasa amejitokeza na kudai alidhalilishwa kimapenzi na mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump.

Karena Virginia anasema Bw Trump alimwendea alipokuwa akisubiri gari nje ya ukumbi wa mashindano ya tenisi ya US Open jijini New York mwaka 1998.

Anamtuhumu mgombea huyo kwa kumshika matiti na kutoa matamshi ya kumdhalilisha kwa wanaume wengine aliokua nao kwenye kundi.

Maafisa wa kampeni wa Bw Trump wamepuuzilia mbali madai hayo na kusema ni "hadithi ya kubuni".

"Mwanaharakati wa kisiasa Gloria Allred, katika njama nyingine, kisa cha kujitafutia sifa
akishirikiana na maafisa wa kampeni wa Clinton, anafanya kila juhudi kumharibia sifa Bw Trump. Tumechoka," amesema Jessica Ditto, msemaji wa kampeni wa Trump.

"Wapiga kura wamechoshwa na vituko hivi na wanakataa hadithi hizi za kubuni ambazo ni wazi kwamba zimekusudiwa kumfaidi Hillary Clinton."

Bi Virginia, ambaye ni mwalimu wa yoga eneo la New York, anasema alitarajiwa kushambuliwa na Bw Trump baada ya kujitokeza lakini kwamba anahisi ni wajibu wake kama "mwanamke, mama na binadamu na raia wa Marekani kuzungumza na kusema ukweli kuhusu" yaliyomtendekea.

"Labda atasema mimi ni mwanamke mwingine mwovu," Bi Virginia ameongeza.

Bw Trump, wakati wa maahalo wa mwisho wa urais wa runinga Las Vegas, alimtaja mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton "mwanamke mwovu sana".
Bw Trump alisema kwenye mdahalo Las Vegas kwamba Bi Clinton ni "mwanamke mwovu sana"

Akiongea kwenye kikao na wanahabari Los Angeles akiwa na wakili wake Gloria Allred, Bi Virginia alisimulia yaliyojiri alipokutana na Bw Trump alipokuwa na umri wa miaka 27.

Anasema alikuwa anasubiri teksi pale Bw Trump alipomwendea na kusema mambo kuhusu mwili na muonekano wake kwa kundi la wanaume aliokuwa nao.

"Alisema: "We, hebu mtazame huyu. Hatujawahi kumuona awali,'" Bi Virginia alisema akitokwa na machozi.

Amesema Bw Trump alimzungumzia kwa wanaume wenzake kana kwamba alikuwa "kitu badala ya binadamu"

"Kisha, mkono wake uligusa sehemu ya ndani ya titi langu upande wa kulia. Nilishangaa sana. Nilishtuka."

Aliambia wanahabari kwamba Bw Trump baada ya hilo alimwabia: "Hunifahamu mimi ni nani?"
"Nilijihisi kudhulumiwa na kama mtu asiye na uwezo," alisema na kuongeza kuwa kisa hicho kilimfanya kujihisi kama mtu "aliyeaibishwa" na kwamba alijilaumu kwa hilo kwa miaka mingi.
Bi Allred, mwungaji mkono mkuu wa Bi Clinton, amesema afisi yake ya mawakili haifanyi kazi na maafisa wa kampeni wa Clinton, na kwamba Bi Virginia ndiye aliyeomba usaidizi wake alipotaka kufanya hadharani tuhuma hizo.

Amesema hakukuwa na mashahidi wengine wa kuunga mkono aliyoyasema Bi Virginia lakini kwamba mwanamke huyo aliwaambia marafiki zake kuhusu yaliyotokea muda mfupi baadaye. Aidha, alimfahamusha mumewe.