Mwenyekiti Yanga akubali amri ya Mahakama

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga ametangaza kuahirisha Mkutano Mkuu wa dhalura wa wanachama, uliokuwa ufanyike kesho tarehe 23 Oktoba, 2016 katika Uwanja wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu hiyo baada ya kukiri kupokea barua ya Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu inayozuia kufanyika mkutano huo, anaandika Kelvin Mwaipungu.

“Jana saa moja tulipata amri ya mahakama ya Kisutu kusitisha mkutano na Yanga inafuata sheria, tusisahau Yanga ilizaa Tanzania kwa hiyo tutatii sheria na agizo la mahakama,” amesema mwenyekiti huyo.

Yanga ilikuwa imepanga kufanya mkutano mkuu siku ya kesho kwa lengo la kujadili namna klabu hiyo itakavyobadili mfumo wake wa uendeshaji kwa kuikodisha timu hiyo kwa Kampuni ya Yanga Yetu kwa kipindi cha miaka 10.

Mwenyekiti wa Yanga amesema kuwa wanachama klabu hiyo waliochukua uamuzi wa kuishitaki mahakamani timu huenda hawajui Katiba yao inasemaje kwani,  ukienda mahakamani unakuwa umejifuta uanachama.

“Wanaoenda mahakamani kutafuta umaarufu wanajiharibia,” amesema.
Zuio hilo limetoka jana jioni baada ya baadhi ya wanachama wakiongozwa na Frank chacha kuiomba mahakama izuie mkutano huo kwani umekiuka utaratibu za uitishwaji ikiwa ni pamoja na uhalali wa siku ya uitishwaji wake.