Mzee Akilimali atishiwa maisha, atoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu mipango inayosukwa juu yake

Mzee Ibrahim Akilimali ambaye ni Katibu wa naraza la wazee wa Yanga SC amesema amesharipoti polisi kutokana na kutishiwa kupigwa ikiwa ni pamoja na kuuawa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kutokana na kutoa maoni yake juu ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu yanayotakiwa kufanywa.

Akilimali ambaye ameripoti katika kituo cha polisi Magomeni, amekwenda pia kwa Mkuu wa Mkoa kumweleza mipango inayoandaliwa juu yake.

“Nimesharipoti polisi na RB ninayo ya kituo cha polisi Magomeni, neno la kusema nitakuumiza, nitakuua huoni kama natishiwa amani, hivi ni nani anayefanya hivi na ni kwasababu ya nani?,” alihoji akilimali alipofanyiwa mahojiano kwenye kipindi cha michezo cha Magic FM ya jijini Dar es Salaam.

“Natishiwa amani, nina RB ndio maana nimekuja kwa Mkuu wa Mkoa kumfahamisha yale matayarisho yaliyoandaliwa kwa ajili yangu. Wewe ndugu yangu unayeshawishiwa kuna nini unachogombea?”

“Mimi nina mawazo yangu na wewe kuwa na mawazo yako, lakini mimi ninachopinga ni mikutano yetu ya Yanga hakuna mkutano ambao wanaweza kukaa watu 500, 1000, 2000, wakaanza kujadili kila mtu akatoa hoja yake, mikutano yetu yakihuni, akishasimama Mwenyekiti akielezea jambo hakuna kupinga.”

Mzee Akilimali akongeza kwamba, kwa matatizo haya yanayoendelea sasahivi ndani ya klabu ya Yanga, kuna mgogoro mkubwa unakuja ndani ya klabu hiyo.

“Mgogoro huu utakuwa mkubwa kuliko migogoro iliyowahi kutokea, sababu kubwa wameingizwa wanachama wanaodaiwa ni wanachama wa posta lakini leo wanaitwa ni wanachama wa Yanga hao wamekuwa wanamgogoro mkubwa, tumewapa jina lao tunawaita ‘Yanga posta’ hawa ndio wamekuwa wachochezi.”

“Sasa natahadharisha, hivi sasa kuna hali mbaya, tungezidisha mshikamano timu yetu nzuri, Mwenyekiti wetu atuite, hakuna wengi wanaotengeneza cha kuwanufaisha wachache, wachache ndio wanaotengeneza cha kuwanufaisha wengi.”

“Vijana wetu wasiingizwe kabisa katika migogoro, majeshi yetu yasiingizwe kwenye migogoro, huu ni mgogoro wa kiutawala, tunakwenda tu wewe usikodishwe, wewe kodisha. Wana Yanga tuwe wenye utulivu, kila mtu apewe uhuru wa kueleza mawazo yake, isiwe kama ilivyojengeka kwamba Mwenyekiti akisema neno basi hilo ndio liwe kama amri ya Mungu, hapana sio demokrasia.”

“Tuwe watulivu, tuwe na amani na tuhitaji maendeleo ya Yanga yetu kwa kujadiliana ili tufikie mwafaka. Mimi nakwenda katika uhuru wa misingi ya uanachama wangu japo nimeshasikia katika watu wanaotarajiwa kufukuzwa siku ya Jumapili mimi ni mmoja wao.”

“Mimi ntakwenda kwenye mkutano licha ya kwamba pameshaandaliwa labda nipigwe au vipi lakini nchi itaona, nchi hii tunatawaliwa na serikali. Kama kutoa maoni yangu ndio sababu ya kupigwa kwangu au kufukuzwa uanachama nchi itaona.”