Posho za Mwenge zilizookolewa kujenga madarasa Malinyi

MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro, Majura Kasika ameagiza posho iliyookolewa kutokana na kufutwa kwa safari ya maofisa watatu na madereva wawili wa wilaya hiyo kwenda kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu mkoani Simiyu, kuelekezwa katika kuongezea nguvu ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo.

Hatua ya viongozi hao kufuta safari hiyo, ilitokana na agizo la Rais John Magufuli aliyeagiza viongozi kutoka mikoa yote nchini, nje ya Simiyu, kutokwenda katika maadhimisho hayo na wale ambao walikuwa tayari wamechukua posho kuzirejesha mara moja.

Kasika alisema jana kuwa kutokana na agizo hilo la Rais, wilaya ya Ulanga iliweza kuokoa Sh 2, 580,000 ambazo sasa zitaelekezwa katika kuchangia ujenzi huo wa vyumba viwili vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi ya Kitongoji cha Lumbanga Kijiji cha Misegesege Kata ya Malinyi.

Akizungumza na wananchi wa kitongoji hicho cha Lumbanga, wakati akiendesha kazi ya uhamasishaji wa uchangiaji wa michango ya maendeleo kwa ajili ya kupata fedha za kuanza kufyatua matofali ya ujenzi huo, Mkuu huyo wa wilaya alisema fedha hizo zitaelekezwa mara moja katika mradi huo.

Uamuzi huo wa Mkuu wa Wilaya, uliungwa mkono na Mbunge wa Malinyi, Dk Haji Mponda ambaye aliahidi kuchangia Sh 500,000 katika mpango huo, huku wananchi wakiahidi kuchangia Sh 30,000 kwa kila kaya.

Kutokana na kijiji hicho kuwa na kaya 400, matarajio ni kuweza kukusanya Sh milioni 12 kutoka kwa wananchi na kufanya jumla ya mchango wa Serikali ya Wilaya na Mbunge Mponda kufikia Sh milioni 15.080, fedha ambazo zitaingizwa katika mradi huo.

Shule ya Lumbanga ni moja ya shule zilizoanzishwa kwa jitihada za wananchi jamii ya wafugaji, ambao wamekuwa wakiishi mbali na shule zilizosajiliwa na hivyo kuamua kuanzisha vyumba viwili vya madarasa vilivyoezekwa kwa nyasi na mabua ya zao la ufuta, kama jitihada za kuwawezesha watoto wao kusoma jirani na maeneo yao.

Mpaka sasa shule hiyo iliyofikia darasa la nne, ina wanafunzi 250 na wanafunzi wake wamekuwa wakionesha uwezo mkubwa katika masomo, ukilinganisha na shule nyingine katika kata hiyo.

Alimtaka pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Malinyi, Marcelin Ndimbwa kuipatia shule hiyo ruzuku ya maendeleo itokanayo na fedha za makusanyo ya ndani pindi watakapokuwa wamefika hatua ya kuezeka na umaliziaji.

Shule hiyo ni mojawapo ya shule za wafugaji ambazo Mkuu wa Wilaya, amedhamiria kuzikamilisha na kuzitafutia usajili.

Shule nyingine ni Mipapa na Likea ambazo zinalelewa na shule mama, lakini zikiwa na walimu wanaojitolea kufundisha.

Wakazi wa kitongoji hicho, walipongeza jitihada zinazofanywa na mkuu huyo wa wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri, wakisema zimeanza kutoa dira ya wilaya hiyo mpya kupaa kimaendeleo kwa kasi inayoendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’.