Tanzania, Morocco kusaini mikataba 11

JUMLA ya makubaliano 11 ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, itasainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Morocco wakati wa ziara ya Mfalme wa Morroco, Mohamed VI.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alibainisha hayo jana wakati akizungumza na waandishi kuhusu ziara ya Mfalme huyo, anayekuja nchini kesho kwa ziara ya kiserikali.

Makonda alisema ziara ya kiongozi huyo, itakiwa na manufaa makubwa kwa nchi, kwani akiwa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli watasaini makubaliano 11 ya ushirikiano katika sekta za kilimo, gesi, mafuta, Reli ya Liganga na Mchuchuma na sekta ya utalii.

Mohamed VI anatarajiwa kufanya ziara ya kiserikali ya siku tano, ambayo ina lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Morroco na Tanzania. Makonda alitoa mwito kwa wakazi wa Dar es Salaam, kujitokeza kwa wingi kumpokea mgeni huyo atakayeambatana na wageni zaidi ya 1,000 na ndege kubwa sita.

Alisema ujio huo utawanufaisha wafanyabiashara wa hoteli ambazo zitatumika kuwahifadhi wageni hao. Aidha Makonda aliwaomba radhi wakazi wa jiji hilo kwa usumbufu watakaopata, kutokana na barabara kadhaa kufungwa siku hiyo ili kuruhusu misafara ya viongozi hao wakuu.

Juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga , alisema ziara rasmi ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco hapa nchini, itaanza Jumapili (kesho).

Baada ya ziara rasmi, atakuwa na likizo na atatembelea sehemu mbalimbali kama matembezi binafsi. Pia, atatembelea Zanzibar na kukutana na Rais Ali Mohamed Shein na pia atatembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA) kwa ajili ya kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Hali kadhalika, mfalme huyo pia atatembelea taasisi za kidini, ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa Kinondoni, na kukutana na viongozi wa dini ya Kiislamu na ataswali sala ya Ijumaa huko Zanzibar.

“Ujio huu ni wa aina yake, mfalme atakuja na watu zaidi ya 150 na miongoni mwao ni wana familia yake na hasa kwa zile siku tano za mwisho, mpaka sasa watu karibu 100 wameshawasili kwa ajili ya maandalizi ya ziara hiyo,” alisema Balozi Mahiga.