Ufisadi wa Sh. 1.3 bilioni kila mwaka Mwanza

HALMASHAURI ya jiji la Mwanza, hupoteza Sh. 1.3 bilioni kila mwaka kutokana na kodi  ya maduka zaidi ya 1024 inayokusanywa kuishia katika mifuko ya baadhi ya wafanyabiashara wajanja na watumishi wa jiji hilo, anaandika Moses Mseti.

Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa jiji la Mwanza ameyasema hayo katika ziara ya kukagua maduka ambayo hayajalipa kodi ya pango mpaka sasa.

Kibamba amesema kuwa baada ya kufika katika jiji hilo miezi miwili iliyopita na kuanza ukaguzi wa miradi pamoja na kupitia mikataba mbalimbali ikiwemo ya maduka hayo, amebaini kuwepo udanganyifu unaoisababishia serikali hasara kubwa.

Amesema kuwa hasara ya zaidi ya Sh. 1.3 bilioni imetokana na watendaji wa serikali katika jiji hilo kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi huku akitolea mfano maduka yaliopo katika shule ya Sekondari ya Pamba tangu mwaka 2006 yaliyoisababishia serikali hasara ya Sh. 350 milioni.

“Ni kitu ambacho hakiingii kwenye akilini tangu mwaka 2006 kampuni ya Lewico inapangisha maduka ya serikali kwa gharama kubwa lakini sisi tunachokipata hakiendani na kinachopatikana.

“Mkataba wa maduka ya serikali unafanyika kati ya shule na kampuni ya Lewico, suala hili haliwezekani na kuanzia sasa hivi mikataba yote itafanywa na halmashauri ya jiji,” amesema Kibamba.
Kibamba amesema kuwa hayupo tayari kuona watu wachache wakijinufaisha kupitia mali za umma na kudai kwamba wote waliohusika katika kuingizia serikali hasara watafikishwa katika vyombo vya dola.

“Sijaja Mwanza kucheza nimekuja kufanya kazi, wanaofanya udalali kwenye mali za serikali waache mara moja na hizo kampuni zao hewa sitaki kuziona katika jiji hili,” amesema Kibamba.

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara katika eneo la Pamba, akiwemo Mashimba Kulwa amesema wanamshangaa mkurugenzi huyo kuwadai mikataba wakati wao waliingia na kampuni ya Lewico.
“Sisi unatuonea bure kwa sababu mkataba wetu tuliingia na kampuni ya Lewico ambayo ndiyo inasimamia maduka yote, kama ni suala la utaratibu kubadilika sisi tutaufuata lakini si kutufungia maduka yetu,” amesema Mashimba.

Hata hivyo MwanaHALISI Online imeona tangazo la tarehe 24 Septemba lililotolewa na uongozi wa kampuni ya Lewico Limited, likiwafahamisha wapangaji wake kuwa jiji la Mwanza halina mamlaka yeyote ya kiutendaji katika mikataba ya maduka hayo.