UN yasikitika Afrika Kusini kujitoa ICC

Hatimaye imethibitika kuwa Afrika Kusini imejitoa kwenye mkataba wa Roma ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, (ICC).

Afrika Kusini iliripotiwa kuwasilisha barua mbele ya Umoja wa Mataifa ikieleza kuwa imefikia hatua hiyo kwa sababu kuwa mwanachama wa ICC kukinzana na sheria ya nchi hiyo ya haki na kinga za kidiplomasia.

Akizungumzia hatua hiyo mbele ya wanahabari mjini New York, Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amethibitisha kupokea barua hiyo na sasa inashughulikiwa na idara ya masuala ya sheria.

Dujarric amesema kuwa Katibu Mkuu Ban Kin Moon amesikitishwa sana na uamuzi wa serikali ya Afrika Kusini kwa kuwa nchi hiyo ilikuwa na mchango mkubwa ICC kwa kuwa ilikuwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kutia saini mkataba huo.

Uamuzi huo wa Afrika Kusini unamaanisha kuwa mwaka mmoja kuanzia sasa nchi hiyo haitakuwa tena mwanachama wa ICC.