Vita ya Lema, wateule wa Rais yafika pabaya

Vita ya kisiasa kati ya Godbless Lema na wateule wa Rais imefika pabaya baada ya Mkurugenzi wa Jiji, Athuman Kihamia kudai kuwa mbunge huyo wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema amemdhalilisha kwa kudai ‘ameolewa na mkuu wa mkoa huo’, Mrisho Gambo.

Kihamia alitoa ‘mashtaka’ hayo jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) alipoomba nafasi ya kufafanua hoja zilizotolewa na Lema na Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro kuwa hawezi kutoa uamuzi hadi apate ushauri kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Katika kikao hicho ambacho Lema, Lazaro na Gambo walihudhuria, Kihamia alisema mbunge huyo alimdhalilisha Oktoba 19 katika kikao cha kamati ya mipango miji.

Mkurugenzi huyo alisema kauli hiyo ilimdhalilisha sana mbele ya watumishi wake, lakini ameamua kuwasamehe na ataendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Mbali ya tukio hilo, Mkurugenzi huyo alisema amekuwa akidhalilishwa kwenye vikao na viongozi hao lakini kamwe hawezi kuacha kutekeleza wajibu wake na akakiri kwamba ni kweli amewazuia wakuu wa idara kuwasiliana moja kwa moja na madiwani.

Akifafanua hoja hiyo, Mkurugenzi huyo alisema kanuni ya 70 (i-v) na kanuni ya 71 zinaeleza wazi kuwa madiwani katika masuala ya utendaji wanapaswa kuwasiliana na mkurugenzi na siyo mtendaji mwingine.