Vyeti 900 vya elimu vyapotea

Zaidi ya matangazo 900 ya kupotelewa vyeti vya elimu yametangazwa kwenye magazeti ndani ya siku 20.

Hiyo inaonyesha kuwa uhakiki wa vyeti vya elimu unaofanywa na Serikali umewatia kiwewe baadhi ya watumishi wa umma na hata wa sekta binafsi na wengi wao sasa wanalazimika kutoa matangazo ya kupotelewa na nyaraka hizo za taaluma kwenye magazeti.

Baada ya Rais John Magufuli kuagiza uhakiki kwa watumishi wote wa Serikali ili kubaini walio hewa, kazi hiyo ilikwenda sambamba na uchambuzi wa taaluma.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Digital umebaini kuwapo kwa idadi kubwa ya watumishi waliotangaza kupotelewa vyeti katika magazeti.

Mwandishi amepitia magazeti manne ya kila siku ya Kiswahili na kubaini kwamba tangu Oktoba Mosi mpaka 21, watu 908 walikuwa wametangaza kupotelewa na vyeti ikiwa na maana kwamba kwa wastani, kila mwezi kuna matangazo kama hayo yapatayo 1,000 magazetini na tangu Januari, watu 10,000 wametangaza.