Zitto Kabwe amemjibu Waziri Nape hoja 7 kuhusu Muswada wa Habari


Kupitia mtandao wa facebook wa Zitto Kabwe, Zitto amejibu haya Kwa HOJA za Nape Nnauye kuhusu muswada wa Huduma za habari, 2016.Tokeo la picha la zitto kabwe

"Anatengenezwa Mhariri Mkuu wa Taifa

Majibu yangu Kwa HOJA za Nape Nnauye kuhusu muswada wa Huduma za habari, 2016

Ndugu yangu Nape Nnauye amejibu andiko langu nililolitoa Jana kuhusu muswada tajwa. Kama ilivyo ada ya Siasa zisizo na Hoja, Nape amejibu andiko langu Kwa kunishambulia binafsi na kuweka Hoja zake mbalimbali. Mimi sitamjibu Nape namna yake maana wenye busara wametufunza Kuwa "When they go Low, We go high" (Wakifanya Siasa Duni, Mwapuuze Na Mfanye Siasa Imara).

Nitajibu Hoja za Ndugu Nape, sitamjibu Nape Juu ya Vijembe, Kashfa na Matusi aliyotumia Dhidi Yangu. Ieleweke kuwa hata kwenye andiko langu la mwanzoni Juu ya Mswada huu (Linapatikana kwenye Ukusara huu) sikutamka neno Nape Nnauye, nilijikita kwenye Hoja tu juu ya Ubaya wa Mswada huu kwa Taifa letu. Kwani Siasa zangu na za Chama changu sio Siasa za mtu bali za masuala. Sitahangaika na mtu bali Hoja ili kujenga.

• Hoja Na. 1: Kushirikishwa wadau: Nape anasema

"Utungaji wa mswaada kuna hatua mbili za kutoa maoni. Hatua ya kwanza ni pale ambapo serikali inapokuwa inatengeneza mswaada husika kabla ya kuupeleka kwenye vikao vya kiserikali kwa hatua za kuupitisha, wadau HUSHIRIKISHWA ili kutoa maoni yao.

Na kwa mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari ,2016 WADAU wameshirikishwa tena na ushahidi wa maandishi wa ushiriki wao na maoni yao UPO.

Hatua ya pili ya utoaji maoni huwa ni baada ya mswaada kusomwa mara ya KWANZA bungeni, Mswaada husika hukabidhiwa kwa Kamati husika ya Bunge, na ukishakabidhiwa huwa ni waraka huru kwa umma kuusoma na kutoa maoni yao (public document) kwa Kamati ya Bunge.

Hili pia limefanyika mpaka hatua ya wadau kuitwa na kuja Dodoma ambapo waliomba mbele ya Kamati wapewe muda wakamilishe kazi ya kusoma na kutoa maoni yao. Na Mwenyekiti wa Kamati Ndugu Peter Serukamba (mb) kwa uamuzi wa Kamati ya kudumu ya Bunge wakaamua kuwaongezea muda wadau kwa wiki moja kukamilisha kazi hiyo, shughuli inayoendelea sasa"

*Majibu yangu juu ya Hoja hii:

Kanuni za Bunge (Kanuni ya 84) zinataka kwamba Muswada ukishasomwa Kwa mara ya kwanza, Bunge lifanye MATANGAZO Kwa umma ili kuhakikisha kuwa umma unaelewa maudhui ya muswada na kuwezesha Wananchi kutoa maoni Yao. Hili halikufanyika, nitathibitisha kwa Hoja.

Kwa Muswada huu, kwanza Bunge halikutoa matangazo yeyote. Kwa Taarifa tu Ni kwamba Hata Kamati ya Bunge (ambayo mimi ni mjumbe) ilishindwa kutoa Nakala (photocopies) za uchambuzi wa muswada kutoka Kwa Wanasheria wa Bunge Kwa sababu Bunge halina Fedha. Wabunge tulielezwa tutumie simu kusoma 'Softcopy' ya Muswada husika Kwa Kuwa Bunge halina Fedha kutoa Nakala Ngumu (Hardcopies) ya nyaraka za Muswada kwa Wabunge ili kufanyia Kazi.

Wadau wote waliokuja mbele ya Kamati ya Bunge walitamka dhahiri kwamba wamepewa Taarifa ya kutokea mbele ya Kamati yetu Siku Mbili (2) kabla ya vikao Na hivyo wameomba muda zaidi wa kutoa maoni Yao.

Labda Ni kutokana Na uchanga wa shughuli za Bunge, Waziri anajenga Hoja kwamba Ushiriki ulianzia kabla. Mtu yeyote anayejua namna Bunge linavyofanya Kazi atakwambia Kuwa muswada ni muswada Tu pale ambapo umechapishwa kwenye gazeti la Serikali Na kusomwa mara ya kwanza Bungeni.

Wadau wote waliiambia Kamati kwamba Kwa muswada huu Ndio walikuwa wanashirikishwa Kwa mara ya kwanza pale mbele ya Kamati. Hivyo wadau hawakushirikishwa kwenye muswada huu tangu umesomwa Kwa Mara ya kwanza Bungeni. Kama Serikali ina ushahidi wowote ule kwamba kati ya Septemba na sasa muswada huu umehusisha mdau yeyote waweke wazi uthibitisho huo.

Nyaraka zinazoonyeshwa Na Serikali Ni za miaka ya nyuma kabla ya muswada kuwa muswada. Ushirikishaji unaanza rasmi pale muswada Unapochapishwa (Kuwa gazetted) Na umesomwa Bungeni.

Hoja Na. 2: Serikali kulazimisha vyombo vya Habari nchini kujiunga na TBC: Waziri Nape anasema
"Mosi, hakuna kifungu kama hicho katika muswada huu. Pili, hakuna dhamira hiyo kwenye muswada huu, na tatu, serikali haina hata wazo hilo".

* Majibu yangu Juu ya Hoja hii

Itakumbukwa kuwa muswada wa awali ulikuwa Na kifungu hiki Na wadau wakapiga kelele sana kukataa. Ukisoma muswada huu Kwa juu juu utaweza kuona kuwa kifungu hiki hakipo. Mtu mwenye dhamira ovu huficha huficha mambo yake. Kwenye muswada huu mambo mengi yaliyokataliwa Na wadau mwanzoni sasa yamewekwa kiujanja Kwa kuweka Mamlaka hayo Kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari.

Serikali inaposema hakuna kifungu hicho haisemi kuna kifungu gani. Nitawaeleza kifungu kilichowekwa ambacho ndicho kitatumika na Waziri kufanya haya (ya kushurutisha Vyombo vyengine vya Habari kujiunga na TBC) bila kuhojiwa Na mtu yeyote yule, kupitia kanuni.

Sehemu ya 7(1)(b)(iv) ya Muswada huu inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari Fulani au masuala Fulani yenye umuhimu kwa Taifa.

Serikali itatumia kifungu hiki kutekeleza jambo lile lile ambalo wadau walikataa kuwekwa kwenye sheria Siku za nyuma. Serikali italiweka Kwa mlango wa nyuma. Mbaya zaidi muswada unatamka wazi kwamba Waziri mwenye dhamana ataweka 'TERMS and CONDITIONS' kwa uendeshaji wa 'media houses' (Vyombo vya Habari).

Hivyo Hata wakifuta kifungu Hicho cha 7, bado Waziri kapewa Mamlaka makubwa sana ya kuamua Chombo cha habari kinaendeshwaji. Ni dhahiri kwamba Waziri ama anajua haya au kawekewa vifungu ambavyo yeye binafsi hajui tafsiri zake lakini atashangazwa katika utekelezaji wa sheria.

Kifungu cha 60(2)(a) kinachosema (Minister to make regulations for TERMS and CONDITIONS for OPERATIONS of licensed media house) kinampa Mamlaka hayo Waziri kiasi ambacho ataweza kuendesha vyombo vya habari atakavyo yeye. Muswada huu unamfanya Waziri wa Habari kuwa Mhariri Mkuu wa Taifa.

• Hoja Na. 3: Serikali Kudhibiti Mitandao ya kijamii: Waziri Nape anasema

"Muswada huu unakusudia kuzibana blogs na kutaja mitandao ya kijamii kama jamiiforums kuwa nayo itatakiwa kusajiliwa. Mtu huyu ni wa kumwonea huruma. Bahati mbaya muswada huo hauna mamlaka wala nia hiyo. Kifungu cha 3 cha Sheria kiko wazi kuwa usajili utahusu magazeti na majarida na machapisho yao ya mitandaoni (magazeti mtandao ya magazeti hayo rasmi na sio mitandao yote au mingine ya kijamii kama anavyopotosha)".

* Majibu yangu Juu ya Hoja hii

Muswada uliopo mbele ya kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana sana ya vyombo vya habari. Sehemu ya 3 ya Muswada inatamka chombo cha habari ni pamoja na gazeti, kituo cha radio na televisheni ikiwemo mitandao ya kijamii (online platforms).

Napenda umma wa Watanzania ufahamu kwamba muswada Ni wa Kiingereza. Muswada wa Kiswahili ni kwa ajili tu ya kuwezesha Wabunge wasiojua kiingereza kuweza kuelewa vifungu vya muswada. Muswada Ulio kwa Lugha ya Kiingereza ndio Muswada rasmi. Mahakamani wakati wa kutafsiri Muswada huu hawatatumia muswada wa Kiswahili Bali muswada rasmi wa Kiingereza.

Tafsiri ya online platforms haikuwekwa kwenye muswada. Tafsiri ya media ndio imeweka Hilo la online platforms. Naomba mtu yeyote akatafute tafsiri Rasmi ya 'online platform' atapata tafsiri Ni Nini. Nitsaidia kidogo hapa

Social media is defined as “online interactions among people in which they create, share, and exchange information and ideas in virtual communities, networks and their associated platform”
Serikali itatumia tafsiri hii ya kwenye muswada kubana mitandao ya kijamii. Hivi Watanzania mmesahau kesi ambazo Wananchi wanapewa kupitia sheria ya cyber crime? Wakati Wabunge walipolalama Bungeni Juu ya Namna Sheria hii itakavyotumika Kubana Uhuru wa Maoni wa Wananchi Serikali ilitoa Majibu ya kupumbaza Kama Haya ya sasa. Lakini sote tunajua hali Halisi ilivyo sasa.

Kiongozi Mkuu wa Serikali (Rais) ameshaonyesha Dhamira Mbaya Juu ya Mitandao ya Kijamii aliponukuliwa kuwa "anatamani mitandao ya kijamii Malaika washuke waizime". Mimi nawaambia Watanzania wenzangu, Malaika watashuka Kwa kupitia muswada huu. Muswada huu una nia ovu kabisa ya kukandamiza uhuru wa habari na Kuzima Mitandao ya Kijamii.

• Hoja Na. 4: Muswada umempa Mamlaka Makubwa mno Waziri wa Habari: Waziri Nape anasema

"Ipo hoja ya Waziri kupewa mamlaka kuagiza chombo chochote kutangaza jambo lenye umuhimu kwa umma: Katika hili pia tumsamehe (Zitto) kwa sababu hahudhurii vikao vya Kamati wakati wa mijadala hii. Hili limejadiliwa kwa kina na wahusika kuelewana. Hakuna kifungu kinachompa mamlaka hayo Waziri.

Bali kifungu kilichopo kinaipa fursa Serikali kuvishauri/kuvielekeza (Government MAY) vyombo vya habari kuungana pamoja kulinda maslahi ya Taifa kunapokuwa na jambo la muhimu kama vile nchi kuwa VITANI au majanga makubwa. Zitto kama kijana wa Kitanzania kama haoni umuhimu wa hili basi hakuna namna nyingine ya kumsaidia".

* Majibu yangu Juu ya Hoja hii

Msomaji utaona dhahiri kuwa hakuna Hoja ya kujibu hapo. Hivi CNN inaagizwa kisheria Na Serikali ya Marekani kuhusu kulinda Nchi Yao? Hivi hapa Tanzania kuna Chombo cha habari binafsi ambacho kinaweza kwenda kinyume Na Nchi wakati wa vita? Muswada umetaja vita?

Maelezo ya Waziri yanaonyesha dhahiri kuwa Serikali haina Hoja bali inahangaika kuokoteza Hoja. Hakuna Ushahidi wa Vyombo vya Habari Binafsi kwenda Kinyume Na Nchi Wakati wa Masuala muhimu ya Kitaifa. Tumeona Vyombo vya Habari Binafsi vikiwa Bega Kwa bega na Maslahi ya Taifa Wakati wa Majanga Kama Ajali ya Meli ya Spice Islanders, Urushwaji wa Matangazo ya Moja Kwa Moja ya Bunge (Kabla haujazuiwa Na Serikali) Na Hata Juzi kwenye Tetemeko la ardhi Bukoba.

Hivyo Serikali HAINA Sababu yoyote ya Kuwa na Kipengele Husika kwenye Muswada.

• Hoja Namba 5: Muswada unampa Waziri wa Habari majukumu ya kutoa masharti kwa kazi za vyombo vya habari na kwamba anaweza kuamua gazeti lichapishwe habari aitakayo: Waziri Nape amesema nimepotosha

* Majibu yangu kwenye Hoja hii

Nimeeleza huko juu (Hoja Namba 2) kuhusu Mamlaka haya ya Waziri wa Habari. Kifungu cha 60 kipo wazi sana.

• Hoja Namba 6: Kuzuia Vitabu na Machapisho Mbaliambali: Waziri Nape anasema

"Zitto anasema muswada huu unampa mamlaka Waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe nchini. Ni kweli muswada umetoa mamlaka hayo lakini Zitto ameamua kutosema ukweli wote.

Muswada unampa Waziri mamlaka hayo si kwa kila jarida au kitabu bali yale tu ambayo yamedhihirika kuchapisha habari huku yakivunja sheria za nchi. Kama Zitto anafikiri nchi yetu itaruhusu majarida yanayotaka kuhamamsisha vita na uvunjifu wa amani nchini, ajue hakuna nchi inayoruhusu mambo hayo".

* Majibu yangu Juu ya Hoja hii

Nadhani wenye uelewa wanaelewa maana ya hili. Sina maelezo ya kujibu hili kwani Majibu ya Waziri yamejitosheleza.

Nani anatafsiri maslahi ya umma? Nani atafsiri kuwa sheria za Nchi zimevunjwa Kama sio Mahakama? Kwanini kabla ya Waziri kufungia vitabu au magazeti asipate amri ya Mahakama? Yeye Waziri Ni Nani Mpaka atoe tafsiri ya kitabu Fulani au gazeti Fulani limevunja sheria?
Tujiulize Watanzania Wote.

• Hoja Na. 7: Kuzuia Uhuru wa Maoni Kwa Kisingizio Cha "Uchochezi": Waziri Nape anasema

"Zitto anazungumzia kuwepo kwa vifungu vya uchochezi akitoa tafsiri kuwa wabunge wa upinzani watabanwa. Kwanza katika hili lazima ijulikane kuwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Kimataifa Juu ya Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966, masuala yote yanayohusu kusababisha athari kwa usalama wa taifa ni ukomo unaokubalika wa uhuru wa habari (allowable restriction to press freedom)".

• Majibu yangu Juu ya Hoja hii

Sina maelezo katika hili. Wenye uelewa wanaelewa namna Hoja za namna hii hutumika. Kiufupi masuala yote ya uchochezi yaliyokuwa kwenye sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 yamerudishwa kwenye sheria hii mpya.

Sheria hii inakwenda mbali Na kusema "Hata ukitamka jambo ambalo linaweza kujenga chuki ya Wananchi dhidi ya Serikali Ni uchochezi".

Mfano Kwa sasa Hakuna Madawa Hospitalini, Serikali imewatelekeza Watoto wa Watanzania Masikini Na Wanyonge Kwa Kuwanyima Mikopo ya Elimu ya Juu zaidi ya Vijana 66,000 Kwa kudai haina Fedha Lakini ikiilipa Mabilioni ya Fedha Kampuni ya Kifisadi ya IPTL kupitia Akaunti ya #TegetaEscrow. Haya Ni Mambo yanayowagusa Na kuwachukiza Wananchi, Ni mambo yanayowaonyesha Kuwa Serikali ya CCM haina dhamira Njema nao.

Nikiyasema Maneno hayo, Na Magazeti yakaandika, Basi Waziri atakuwa na Mamlaka ya Kutafsiri Huo ni Uchochezi Na kulifungia Gazeti Husika. Hii ndio Hatari ya Mswada huu.

• Muhimu Sana

Napenda kutoa ushauri wa bure Kwa Ndugu Yangu Nape Nnauye, kwamba kujadiliana Kwa Hoja kuna Maslahi Kwa Nchi. Wote waliosoma andiko langu (la Awali, Na Hata hili) wataweza kutofautisha Vijembe, Dharau, Kulewa Madaraka Na Matusi kwenye majibu ya Nape Na Hoja, Staha na Heshima kwenye andiko langu.

Katika andiko langu (la awali) sikumtaja Nape Kwa jina Kwa sababu najua anatimiza wajibu wake Kama Waziri. Katika majibu yake kuanzia mwanzo Mpaka mwisho Ni vijembe tu. Hii inaonyesha uwezo wetu mdogo wa kuhimili mijadala. Hii Ndio inayofanya Watanzania tuonekane watu ambao hatukusoma au tulikwenda shule lakini hatukuelimika.

Haiwezekani kwamba mtu yeyote ambaye ana Hoja tofauti Na wewe atakuwa ametumwa. Kwamba hatuna uhuru wa mawazo binafsi Na hivyo lazima tutumwe. Hii Ni hulka mbaya sana ambao sikutegemea Kama wanasiasa vijana wanaweza kuiendeleza. Lakini Kama kuna mtu ambaye amezoea kutumwa Hoja Ni dhahiri kwamba anaona mwengine yeyote mwenye Hoja nyengine katumwa Pia.

Kwa Dhati Ninaamini muswada huu Ni mbaya Na unadidimiza uhuru wa habari. Ninaamini kuwa muswada huu Kama ulivyo haupaswi kujadiliwa Na Bunge Kwa sababu unapaswa kuandikwa upya.
Muswada huu ukipitishwa hakuna mchapishaji (Printing Company) wa magazeti atakayekubali kuchapisha magazeti Kwa sababu Kwa mujibu wa muswada Mkurugenzi wa Maelezo anaweza kuingia kwenye mtambo wowote wa Kuchapisha Magazeti akiwa Na Polisi Na kuung'oa Kwa Kuchapisha Tu Gazeti lenye Habari zisizoipendeza."

Mimi nimeandika. Nimetahadharisha. Nimetimiza wajibu wangu.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto

Njiani kwenda Maputo Kuadhimisha Kifo Cha Komredi Samora Machel
Oktoba 21, 2016