Jinsi ya kupata ngozi laini

Takribani kila mtu angependa kuwa na ngozi laini, au hata laini zaidi. Watu wengi wamekuwa wakiitafuta ngozi nzuri au kujitahidi kuitunza ili isiharibike. Lakini je, wamefanikiwa?

Wachache hufanikiwa na wengi hushindwa. Na hata hao waliofanikiwa wengi wao hutumia vipodozi vikali ambavyo vingi huchubua na kuharibu ngozi zao na kuwaletea madhara makubwa sana baadae. Vipi wewe, ungependa kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako? Karibu somo la leo ili uweze kuwa na ngozi nzuri bila kuidhuru afya yako.

Ngozi laini ni nzuri na inaongeza mvuto wa mwili. Ulaini wa ngozi hupotezwa na mambo mbalimbali kama vile seli za ngozi kupungukiwa na maji na kuanza kusinyaa na kunyauka, seli za ngozi kujeruhiwa,  na seli za ngozi kufa. Matokeo yake ni michirizi, makunyanzi, makovu, chunusi, madoa, ngozi kufubaa na kuzeeka.

Kuifanya ngozi kuwa laini unahitaji kuupatia mwili virutubisho vyote vya kujenga mwili vizuri na kunywa maji ya kutosha ili seli zisikauke, kusinyaa wala kunyauka. Kula mlo kamili, matunda mengi na kunywa maji ya kutosha.

Pia unahitaji kuepuka jua kali ambalo litaunguza ngozi, kuikausha na kuifanya iwe na makunyanzi na vitu vingine vinavyoota kwenye ngozi kutokana na jua.

Tumia vipodozi vizuri vinavyosaidia ngozi kuwa laini bila kuidhuru. Hapa kuna vipodozi vya aina mbali mbali na vinavyofanya kazi kwa njia mbali mbali. Vipodozi vya muhimu ni


  1. Vipodozi vya kuongeza unyevu au maji kwenye (seli za) ngozi
  2. Kwa kiingereza vinaitwa “Moisturizers”. Hivi hufanya kazi ya kufunika ngozi na kuzuia maji yasipotee kutoka kwenye ngozi, na pia husaidia kuongea maji kuingia kwenye seli za ngozi. Vipo katika mtindo wa sabuni, mafuta na losheni.
  3. Vipodozi vya kusaidia kuongeza kasi ya kuzalishwa kwa seli mpya za ngozi
  4. Hivi husaidia kuzalisha seli mpya za ngozi ambazo zitaleta ngozi mpya na nzuri na kuondoa ile ya zamani iliyochoka na kuzeeka. Mifano ni losheni na krimu zenye Vitamini A na Vitamini E.
  5. Vipodozi vya kusaidia kuondoa uchafu na seli (ngozi) zilizozeeka au kufa

Tumia sabuni zenye uwezo mkubwa wa kuondoa uchafu kutoka kwenye ngozi, na ukiweza tumia “face wash” au “facial cleansers”. Hivi husaidia kusafisha kabisa ngozi na kuondoa uchafu.

Kwa upande wa seli zilizokufa na kubaki juu ya ngozi tumia “scrub”.  Scrub hufanya kazi kwa kuondoa seli zilizoharibika na zilizokufa na kuacha seli changa na ngozi nzuri.

USHAURI :


  1. Pata ushauri wa kulainisha na kupendezesha ngozi yako kutoka kwa wataalam wanaojua vizuri afya, urembo na vipodozi. Utashauriwa vizuri jinsi ya kufanya, vipodozi vya kutumia na jinsi ya kuvitumia vizuri kwa matokeo mazuri zaidi. Epuka wauza vipodozi wasio waaminifu au wasiovijua vizuri vipodozi, maana wanaweza kukupa vipodozi vya tofauti na mahitaji yako au vipodozi vinavyodhuru afya yako.
  2. Safisha ngozi yako vizuri, kila siku. Hakikisha unaondoa uchafu na vijidudu vyote vinavyotua na kukaa juu ya ngozi yako. Ondoa vumbi, seli zilizokufa, mafuta ya ziada, jasho nk Lala na pumzisha ngozi yako kiasi cha kutosha ili iweze kujitengeneza na kuwa nzuri. Ipumzishe kila siku kwa matokeo mazuri zaidi. Pata usingizi wa kutosha na ulio bora
  3. Tumia vipodozi vizuri vyenye uwezo wa kukupa matokeo mazuri unayoyataka na visivyodhuru afya yako. Pata ushauri mzuri kutoka kwa wataalam ili uweze kufanikisha hili vizuri. Tumia vipodozi vinavyoendana na ngozi yako. Kama ngozi yako ni kavu tumia vipodozi ambavyo ni maalum kwa ajili ya ngozi kavu, na kama ngozi yako ni ya mafuta basi tumia vipodozi ambavyo ni mahususi kwa ajili ya ngozi ya mafuta.
  4. Usitumie vipodozi vinavyoharibu ngozi na kuihatarisha ngozi yako. Epuka vipodozi vyote visivyo salama na vile visivyoendana na ngozi yako.
  5. Jihadhari na michubuko au majeraha mengine yoyote yatakayoweza kuharibu ngozi yako. Hii ni kwa sababu michubuko na majeraha hayo yatakuharibia uzuri wa ngozi yako na pia yatakuachia makovu baada ya kupona
  6. Kuwa na furaha, amani na tabasamu itakusaidia pia kuwa na ngozi nzuri, hususan ngozi ya usoni.