Kauli ya Wazee Simba kaa la moto

Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa Simba, Mzee Hamisi Kilomoni (kulia) akizungumza na wandishi wa habari kuhusu kutotambua kuitishwa kwa mkutano wa dharula wa timu hiyo jijini Dar es Salasam jana. Kushoto ni Katibu wa Baraza la Waasisi wa Simba, Malik Snous. Picha na Said Khamis 

Dar es Salaam. Kauli ya Baraza la Wadhamini la klabu ya Simba kuzuia mkutano ulioitishwa na uongozi, ushiriki wa Simba katika Ligi Kuu ni kati ya mambo yaliyotawala mkutano wa jana wa viongozi wa matawi na uongozi.

Mkutano huo umekuja ikiwa ni siku moja baada ya Mwenyekiti wa baraza hilo, Hamis Kilomoni kutangaza kuwa hawautambui mkutano wa Simba ulioitishwa na uongozi huo wa klabu hiyo Desemba 11.

Mkutano huo umeitishwa kwa ajili ya kufanyia marekebisho Katiba ya Simba ili kumpa nafasi Mohamed Dewji (MO) kuwa na uhuru wa kununua hisa 51 na wanachama kubaki na 49 hatua inayopingwa na baraza hilo kuwa halikushirikishwa katika kufikia uamuzi huo.

Viongozi wa matawi wakutana

Viongozi wa matawi ya klabu hiyo mkoani Dar es Salaam walikutana na kubwa ni kujadili kauli ya wazee na ushiriki wa timu hiyo katika Ligi Kuu kuelekea mzunguko wa pili.

Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Kaburu alisema kikao hicho ni cha ndani na chenye lengo la kuweka mikakati kwa ajili ya ushiriki wa klabu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

“Waandishi mtupishe, hiki ni kikao cha ndani.Tunajua wengine ni upande wa pili, tukisema hapa yatafika mara moja,” alisema Kaburu.

Kabla ya waandishi kutimuliwa rais wa Simba, Evabs Aveva alitambulisha agenda mbili katika mkutano huo ambazo ni kujadili ushiriki wa timu hiyo katika mzunguko wa pili na mkutano mkuu wa dharura uliopangwa kufanyika Desemba 11.

Awali tofauti na ilivyofikiriwa kuwa kungetokea fujo baada ya baraza hilo kubainisha hivyo viongozi wa matawi walianza kuingia makao makuu ya klabu saa 7:30 mchana wakiwa katika nyuso za furaha na kutaniana.


Wanachama wanena

Baada ya waandishi wa habari kuondolewa kwenye kikao hicho, gazeti hili lilizungumza na wanachama wa klabu hiyo waliokuwa nje ya makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi huku wakiwa na mitazamo tofauti kuhusu agenda za kikao.

“Suala la ushiriki wa timu katika mzunguko wa pili lipewe kipaumbele, hatukumaliza vizuri mzunguko wa kwanza. Wanasimba tunataka furaha safari hii,” alisema Muddy Mabegi mwenye kadi namba 28140

Amina Poyo alisema: “Tunachotaka utaratibu ufuatwe, kikao cha viongozi wa matawi kitatupatia mrejesho ambao tutakwenda nao kwenye mkutabo mkuu.”

Mpaka gazeti hili linaondoka makao makuu ya klabu hiyo kikao kilikuwa kinaendelea na taarifa zilisema viongozi wa matawi licha walijadili kwa kina agenda zilizowasilishwa, suala lililokuwa zito ni kuhusu umilikishwaji wa hisa za MO.