Kibaigwa wakimbia kulazwa hospitali kwa kuhofia kurogwa



Dodoma.  Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Kibaigwa wanaougua kipindupindu wanadaiwa kukwepa kwenda hospitali kutokana na imani potofu kuwa wakilazwa watarogwa.

Akizungumza na wenyeviti wa vijiji na vitongoji, Ofisa Afya Mkuu wa Mazingira, Carle Lyim alisema tabia ya kujitibu nyumbani inatokana na mila potofu kuwa wakilazwa maadui zao watapata nafasi ya kuwaondoa uhai pindi wanapokwenda kuwaona.

Alisema katika Kijiji cha Tubugwe walibaini kuwapo kwa familia 21 ambazo zimehifadhi dawa nyumbani kwa ajili ya kujitibu.

“Tulitoa elimu kwa wakazi wa eneo hilo na kuunda timu ili kubaini chanzo cha kipindupindu katika eneo hilo na hadi sasa hakuna kesi nyingine,” alisema.