Kukamatwa kwa watuhumiwa 586 wauhalifu Dar kwazua maswali

Dar es Salaam. Jiji la Dar si salama. Hivyo ndivyo inavyoelezwa na wasomi ikiwa ni siku moja baada ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutangaza kuwakamata watuhumiwa sugu 586 wa uhalifu ndani ya siku 10.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumezua maswali kadhaa ikiwamo usugu wa wahalifu hao, magereza wanazowekwa na usalama wa wakazi wa Dar es Salaam.

Juzi, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro amesema wamewakamata watu hao kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.