Lowassa alikoshwa na aina ya uongozi wa Fidel Castro

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kiongozi wa zamani wa Cuba, Fidel Castro alikuwa anamvutia na kwamba ni mfano unaofaa kuigwa kutokana na kuwa mstari wa mbele kusaidia mataifa maskini ili yaendelee.

Castro, ambaye alifariki Novemba 25, anajulikana kwa siasa zake za mrengo wa kushoto akiwa amepambana na ubepari kwa kipindi chote cha uongozi wake wa Taifa la Cuba aliloliongoza kwa miaka 47 akiwa kwanza kama Waziri Mkuu (1959-1976) na baadaye rais kuanzia mwaka 1976 hadi 2006 alipoachia ngazi.

“Kwangu Castro ni kiongozi wa mfano. Ni kiongozi aliyenivutia ambaye kazi aliyoifanya si tu imeacha heshima nchini mwake, bali pia katika mataifa mbalimbali duniani,” Lowassa alisema jana akiwa nyumbani kwa balozi wa Cuba nchini, Jorge Luis Lopez alipokwenda kutia saini kitabu cha maombolezo ya kiongozi huyo.