Majaliwa: Hatutamvumilia mtumishi atakayeleta urasimu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amesema serikali inahitaji ushirikiano wa wafanyabiashara, hivyo haitakubaliana na mtumishi yeyote wa umma atakayefanya urasimu kwa lengo la kukwamisha uboreshaji wa sekta binafsi.

Alisema miongoni mwa maboresho yanayofanywa na serikali katika sekta binafsi ni pamoja na kuimarisha utendaji wa watumishi na kuondoa urasimu katika utendaji kazi wa kila siku baada ya eneo hilo kulalamikiwa sana.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mkoani hapa, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

Ziara hiyo inalenga kuangalia utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), utendaji wa serikali, kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi wa mkoa huo na kushirikiana na viongozi wa mkoa ili kuweza kuzipatia suluhisho.

“Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi yetu. Pia mapambano dhidi ya rushwa yanayofanyika ndani ya serikali na nje yanalenga kuleta maboresho makubwa katika sekta binafsi ,” alisema.

Alisema serikali inawataka watendaji wake wote watumie lugha nzuri na rafiki katika kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla na haitamvumilia mtumishi yeyote atakayefanya urasimu ili mfanyabiashara atoe rushwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema serikali itaimarisha mipaka yake na kuzuia uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje ambazo nyingi zinazalishwa hapa nchini huku lengo likiwa ni kulinda viwanda vya ndani.