Serikali yaangalia upya utitiri wa kodi

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema serikali inaangalia upya sheria na sera ya taasisi ndogo za fedha zinazowawezesha wajasiriamali wadogo kwa sababu hivi sasa riba itozwayo ni kubwa sawa na zile za mabenki.

Alisema mpango huo una nia ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha na mitaji kwa wajasiriamali wadogo nchini hatua itakayoboresha maisha yao na kukuza pato la taifa.

Aidha, amesema serikali imesikia kilio cha utitiri wa kodi unaotozwa na mamlaka mbalimbali nchini na inaangalia jinsi ya kuzichanganya na ziwe zinatozwa kwa taasisi moja.

Akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo ya usindikaji na ufungashaji vyakula jana jijini Dar es Salaam, serikali imelazimika kuangalia upya sera na sheria za taasisi ndogo za fedha ili kuwainua wajasiriamali wa hapa nchini.

“Nipongeze baadhi ya taasisi za fedha kama benki, lakini kikwazo ni riba tumeona tuangalie upya sheria na sera ya hizi microfinance (taasisi ndogo ndogo za fedha), kwa sababu zinatoza riba kubwa ili hali zinapaswa kutoza riba ndogo kwa wajasiriamali,” alisema Samia.

Akizungumzia hatua walizopiga wajasiriamali katika kuzalisha bidhaa zenye ubora, Samia alisema wasindikaji wadogo wana uwezo wa kusindika bidhaa bora na changamoto ni maeneo ya usindikaji.

Hata hivyo, alishauri Watanzania kuacha tabia ya kuwa wazungumzaji tu bila matendo na kuwataka kufanya kazi kwa bidii huku akitoa mwito kwa taasisi za utafiti nchini kutafiti jinsi serikali inavyoweza kusaidia sekta isiyo rasmi kurasimishwa.

Pia alizitaka taasisi hizo kuangalia viwanda vya usindikaji nchini vinavyotoa mabaki ya aina gani na jinsi ya kuyabadilisha kuwa mali. Kuhusu kodi Makamu wa Rais alisema utitiri wa kodi ni kilio cha wengi na kwamba serikali itahakikisha inalifanyia kazi ili ziwe zinatozwa kwa pamoja.

“Tunapopita kwa watu na wafanyabiashara na hata viwandani kilio kikuu ni uwepo wa utitiri wa kodi zinazotozwa na mamlaka tofauti sasa tunaziangalia jinsi ya kuzichanganya zitozwe sehemu moja,” alisema Samia.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wajasiriamali Wasindikaji wa Vyakula (TAFOPA), Suzan Laizera aliomba kutengwa kwa maeneo ya usindikaji hadi vijijini ili kusaidia wazalishaji kupata vigezo vya kupewa nembo za ubora wa uzalishaji bidhaa.

Mwakilishi kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Lous Akaro alisema ni lazima sekta ya usindikaji iendelezwe iwapo nchi inahitaji maendeleo.

Hivyo alipendekeza maeneo matano yanapaswa kuangaliwa ili kuhakikisha sekta hiyo inakua, moja wapo ikiwa ni kutengwa kwa asilimia 30 kwa ajili ya usindikaji wa viwanda vidogo na wajasiriamali wanawake kwenye Ukanda wa Uwekezaji Nchini (EPZ).