https://monetag.com/?ref_id=TTIb VETA yaombwa ijenge chuo Bagamoyo | Muungwana BLOG

VETA yaombwa ijenge chuo Bagamoyo

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga ameiomba Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kujenga chuo cha ufundi katika wilaya hiyo kwa ajili ya kuwasaidia vijana kujiendeleza wapate ajira.

Akifunga mafunzo ya ufugaji samaki kibiashara yaliyofanyika juzi katika Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kilichopo Mbegani, Bagamoyo ambapo mafunzo hayo yalidhaminiwa na VETA, Mwanga alisema yupo tayari kuipatia mamlaka hiyo eneo kwa ajili ya ujenzi huo.

‘’ Tunaomba Veta Kanda hii ya Mashariki iandike mapendekezo kwenda Makao Makuu yenu kwamba tunaomba kujengewa chuo cha ufundi lengo ni kuwasaidia vijana wetu,’’ alisema Mwanga.

Alisema kuwa pamoja na elimu itakayotolewa watakuwa na uhakika wa kupata maziwa yatakayozalishwa na wanafunzi watakaopata nafasi ya kujiunga na chuo hicho.

Aidha, alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi wilayani humo, watahakikisha kwamba wanatoa eneo hilo kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda hiyo, Asanterabi Kanza, alisema watahakikisha kwamba wanaendelea kufadhili mafunzo hayo ili kukuza masuala ya biashara na vipato binafsi.

Alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), ilisaidia kudhamini mafunzo hayo na kueleza kuwa wahitimu wanatakiwa kutumia mafunzo hayo kuzalisha ajira kwa watu wengine ili kuleta maendeleo.