Wadau waikaanga Wizara ya Mali asili mbele ya Majaliwa

Arusha. Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato) jana kimeilipua Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Profesa Jumanne Maghembe mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kikisema imekuwa ikitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu idadi ya watalii wanaoingia nchini na hivyo kuzipotosha taasisi nyingine za Serikali kufanya uamuzi sahihi.

Wakizungumza katika kikao baina ya Waziri Mkuu na wafanyabiashara mkoani Arusha, viongozi wa Tato, walisema takwimu ambazo zinatolewa na wizara hiyo kuwa Tanzania imepokea watalii zaidi ya milioni moja mwaka jana si sahihi.

Mwenyekiti wa Tato, Willy Chambulo alisema wamekuwa wakipinga takwimu za kisiasa zinazotolewa juu ya ongezeko la watalii, bila ya mafanikio na sasa wanamuomba Waziri Mkuu kuunda kikosi kazi kuinusuru sekta hiyo.

“Sisi ndiyo tunaopokea watalii, hawajawahi kufika milioni moja, tunaomba kawaulize watu wa uhamiaji na wengine watakupa ukweli. Mtalii ambaye anaingia nchini anatakiwa kulipa viza ya dola 50 (Sh64,000) kwa nchi nyingi. Kwa Wamarekani ni dola 100 (Sh128,000), sasa waulizwe Uhamiaji kama wamewahi kupata dola milioni 50 ambazo ni zaidi ya Sh100 bilioni kutokana na viza?

Huku akinukuu taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Chambulo alisema inachofanya ni kuchukua takwimu za kimataifa za watu wote wanaoingia nchini, wakiwamo wakimbizi na wasafiri wa kawaida na kuwaita watalii.