Wakazi wa Mvumi Wadamka usiku wa manane kwenda kuchota maji mtoni kwa njia ya wizi, kukwepa faini ya 50,000.

Wananchi wa kijiji cha Mvumi wilayani Kilosa wanalazimika kudamka usiku wa manane kwenda kuchota maji katika mto Mvumi kwa njia ya wizi ili kukwepa kutozwa faini ya shilingi 50,000 baada ya Serikali ya kijiji hicho kupiga marufuku matumizi ya maji ya mto huo kwaajili ya kunywa na kupikia.

Wamesema Serikali ya kijiji cha Mvumi imepiga marufuku hiyo kwa madai kuwa maji ya mto huo yamekuwa chanzo cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu lakini pamoja na marufuku hiyo uongozi wa kijiji haukueleza njia mbadala ya kuwapatia maji safi na salama ili kuondokana na kero.

Pamoja na kero ya maji wananchi hao wamelalamikia ukosefu wa dawa katika zahanati ya kijiji hicho ambapo wanasema hawaoni faida ya kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF kwasababu kila wakienda hospitalini wanaambiwa hakuna dawa.
 
Wakizungmzia ufumbuzi wa kero hizo wakati wa mkutano na wananchi wa kijiji cha Mvumi, Mbunge wa jimbo la Kilosa Kati mheshimiwa Mbaraka Bawazili na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya kilosa Bwana Hassan Mkopi wameahidi kuchimba visima vya maji ikiwemo kukutana na uongozi wa kijiji hicho kuangalia uwezekano wa kuondoa zuio hilo.

Uchungizi wa ITV umebaini kuwepo kwa kinyesi cha binadamu kandokando yamto ambao wananchi wanachota maji kwaajili ya matumizi mbalimbali hali inayoashiria kuwepo kwa mwamko duni ya matumizi ya vyoo.