Watoto 2 waugua kisukari katika kila wagonjwa 10

WAKATI Tanzania ikitajwa kuwa na wagonjwa 822,880 wa kisukari kwa takwimu za mwaka 2015, imebainika kuwa kundi la watoto lipo katika hatari kubwa zaidi ya kuugua ugonjwa huo endapo wazazi hawatachukua hatua madhubuti.

Uthibitisho huo umewekwa wazi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anayesema kuwa takwimu za watoto wenye kisukari kwa mwaka 2015 ni asilimia 20 ya wagonjwa wote wa kisukari wanaotibiwa kwenye kliniki nchini.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kuwa kati ya wagonjwa 100 wanaotibiwa kisukari nchini, wagonjwa 20 ni watoto sawa sawa na kusema kuwa kati ya wagonjwa 10 ni lazima wawepo watoto 2. Kutokana na takwimu alizotoa Waziri Ummy hivi karibuni kwamba Tanzania ina wagonjwa 822,880 wa kisukari, hivyo kuna watoto 164,000 wanaougua ugonjwa huo nchini kote.

Kwa mujibu wa Waziri, takwimu hizo ni kwa wagonjwa waliofika hospitali lakini akasema wapo ambao kutokana na mila na desturi potofu wanaugua ugonjwa huo bila kufika hospitali na hivyo huenda tatizo ni kubwa zaidi. Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu.

Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin ambayo husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe.

Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hicho kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili.

Maisha ya ‘kizungu’ ni tatizo Akichambua hatari inayowakabili watoto nchini dhidi ya ugonjwa huo wa kisukari jijini Dar es Salaam jana, daktari bingwa wa magonjwa ya kisukari na homoni kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Fadhili Kumbakumba alisema malezi ya kisasa kwa watoto yanawaweka katika hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huo.

Mtaalamu huyo alisema vyakula ambavyo wanapewa watoto, lakini wakishindwa kupata muda wa kucheza michezo inayoweza kushughulisha miili yao, huku wazazi wao wakiona kuwa wanawalea maisha ya kisasa (lugha maarufu maisha ya kizungu) ni chanzo cha watoto wengi kuugua kisukari.

“Mtoto anaamka asubuhi anakunywa chai na mkate umepakwa siagi, karanga za kusagwa, jamu, mayai ya kukaanga, juisi ya viwandani, kisha anakwenda shule na gari la shule au anapelekwa na gari la mzazi lenye kiyoyozi. “Mtoto huyu akifika shuleni ni kusoma tu; na bahati mbaya shule za sasa hazina michezo ambayo watoto wa zamani walikuwa wakicheza. Na akirudi tena nyumbani mtoto huyo anapewa maziwa, na vyakula vingine vya kusindikwa na haruhusiwi kutoka nje kucheza na wenzake,” alisema Dk Kumbakumba.

Katika kile alichosema ni kulelewa kizungu, mtaalamu huyo alisema; “Mtoto anaporudi nyumbani, dada wa kazi anakuwa ameshapewa maelekezo asimruhusu kabisa kutoka nje bali amsimamie afanye kazi za shule na kukaa kuangalia katuni. Usiku ukifika anakula tena mlo kamili na kulala. Hii ni hatari kubwa.” Hali ilivyokuwa zamani Daktari huyo anasema katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuna idadi kubwa ya watoto ambao wana ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza, ambao unawaathiri watoto unaotokana na ama kuzaliwa nao au kujikuta wakiupata mapema kutokana na mazingira hayo ya maisha."

Alisema watoto wa zamani walikuwa wakinywa chai na kipande cha muhogo au kiazi, wanatembea umbali mrefu kufika shule na huko shuleni wanakutana na michezo ya kutosha pamoja na kazi za mikono kama vile ulimaji wa bustani na umwagiliaji.

“Watoto wetu wa sasa tunavyowalea hata maua hawawezi kumwagilia, huwezi kumtuma hata kikombe cha maji, badala yake unamwita dada wa kazi afanye. Mzazi anaona kufanya hivyo ndiyo kumuonesha mtoto mapenzi kumbe anamuua. “Akiamua kumtoa mtoto anampeleka kwenye kucheza gemu za kompyuta na si kucheza mpira atoke jasho au mchezo mwingine wa aina hiyo,” alisema Dk Kumbakumba.

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, hospitali hiyo imekuwa ikiendesha kliniki ya watoto kila siku ya Jumatatu ambapo huwapima na kuwapa huduma mbalimbali za matibabu watoto wenye ugonjwa huo na baadaye kuwatenga katika makundi ili kuwafuatilia kwa karibu zaidi.