Zaidi ya wanafunzi 7,000 kufutiwa udahili vyuo vikuu



TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imebainisha jumla ya vyuo 52 vyenye wanafunzi zaidi ya 7,936, ambao wamedahiliwa katika programu ambazo hawana sifa.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Katibu Mtendaji wa TCU, imesema tume hiyo imekamilisha uhakiki wa sifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye baadhi ya vyuo vya elimu ya juu nchini.

Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa orodha ya wanafunzi wasio na sifa imeshawasilishwa kwenye vyuo husika.

“Hivyo wanafunzi wote wanaoendelea na masomo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini wanaweza kutazama matokeo ya uhakiki wao kupitia tovuti ya tume,” ilisema taarifa hiyo kupitia tovuti ya tume hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TCU, wanafunzi wote waliobainika kukosa sifa hizo, wawasiliane na vyuo vyao ili kuthibitisha sifa zao kabla ya Februari 28, mwaka huu.

“Kwa wanafunzi ambao hawatahakiki taarifa zao vyuoni mwao, hawatatambuliwa na TCU na hivyo kukosa sifa za uanafunzi,” ilifafanua taarifa hiyo. Katika tovuti hiyo, jumla ya vyuo vikuu 52 vilihakikiwa ambapo zaidi ya wanafunzi 7,936 walibainika kudahiliwa katika programu ambazo hawana sifa nazo.

Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (AJUCO) wanafunzi 27, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) 96, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 224, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) 52, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira Kampasi ya Dar es Salaam 74, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)164.

Vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA) 33, Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) 23, Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) 162, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must)11, Chuo Kikuu cha Mzumbe 639 na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) 44.

Vingine ni Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU) 115, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) 1,046, Chuo cha SAUT Arusha mmoja, Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) 150, chuo cha Udaktari cha St Francis Ifakara(SFUCHAS)76 na College of Management and Commerce (SJUCMC) mmoja.

Aidha, vyuo vingine ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo) 15, Chuo Kikuu cha St John’s Tanzani (SJUT) 968, Chuo cha St Marks 129 na Chuo cha Udhibiti na Usimamizi wa Wanyamapori (CAWM) wanafunzi sita.

Katika tovuti hiyo pia vyuo vingine vilivyohakikiwa na kubainika kuwepo kwa wanafunzi hao ni Chuo Kikuu cha SUMAIT 552 na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dodoma 375 na CBE Mwanza 101, Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) 14 na Chuo cha Diplomasia (CFR) 14.

Vyuo vingine ni Chuo cha Bugando (CUHAS) wanafunzi 36, Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Bahari (DMI) wanafunzi wanne, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EAST C) 20, Chuo Kikuu cha Tanga Eckernforde (ETU) watatu na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Herbert Kairuki 12.

Aidha, wanafunzi wengine waliohakikiwa na kubainika kudahiliwa katika programu ambazo hawana sifa nazo walipatikana katika vyuo vya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wanafunzi 56, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) 305, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) 149 na Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) 116.

Vyuo vingine ni Chuo cha Kodi (ITA) wanafunzi sita, Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan (JUCO) 186, Kilimanjaro Christian University College (KCMUco) 55, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Muco) 62, Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA)(20) na Chuo Kikuu cha Bagamoyo wanafunzi 53.

Vingine ni Chuo cha Tumaini Makumira (TUMA) wanafunzi 208 waliokutwa hawana sifa katika programu wanazosomea, TUMA-Mbeya 11, Chuo Kikuu cha Iringa (UOI) 522, Chuo Kikuu Sumait 552, Chuo Kikuu cha Teofil Kisanji (TECU) Dar es Salaam watatu, Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris (STEMMUCO) 44 na Chuo cha Mipango wanafunzi 431.