https://monetag.com/?ref_id=TTIb Kibiti: Hofu yazidi baada ya kusambaa ujumbe wa kuua polisi zaidi | Muungwana BLOG

Kibiti: Hofu yazidi baada ya kusambaa ujumbe wa kuua polisi zaidi

Kibiti. Siku mbili tangu kuuawa kwa polisi wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani ambao walikuwa kazini katika Kijiji cha Bungu B, hali ya wasiwasi imezidi baada ya wauaji hao kusambaza ujumbe unaoeleza kuwa wanaendelea kusaka askari kwa kuwa ni wadhurumaji.

Watu hao wametuma ujumbe mfupi uliondikwa kwenye karatasi na kisha kuutuma katika mitandao ya kijamii, ukidai kuwa waliouawa (japo hawajatajwa majina yao) walidhulumu watu kwa kutumia kazi zao.

“Tunawatangazia wananchi tumewaua hawa kwa sababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hata nyumbani kwake. Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi, kwa hiyo dereva au raia popote uwaonapo toa taarifa iwe nyumbani au kazini,” unasema ujumbe huo.

“Hakuna njia ya kumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa chuma tuuu!”

Ujumbe huo ambao umeandikwa kwa mkono kwa kutumia kalamu ya rangi ya bluu unadaiwa kuwa unazungumzia vifo vya askari polisi wawili wa Kituo cha Polisi Kibiti, Sajent Salum na PC Masola waliouawa kwa kupigwa risasi wakiwa kazini.

Mmoja wa madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti (jina tunalo) alisema ujumbe huo unawalenga askari wa kawaida na wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Diwani huyo alisema kundi hilo linalofanya mauaji katika wilaya za Kibiti na Rufiji bado lipo na lina nguvu.

“Linaonyesha bado lina uwezo mkubwa wa kufanya mauaji na kutokomea kusikojulikana,” alisema.

Alisema kwa sasa Serikali inapaswa kuongeza nguvu zaidi ya wapelelezi ili kukomesha kikundi hicho ambacho hakijajulikana kinafanya hivyo kwa sababu zipi na wala kinakojificha.

Akizungumzia ujumbe huo, kamanda wa polisi wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuwasaka.

“Tutapambana nao tu,” alisema Kamanda Lyanga na kukata simu.

Mkuu w Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro alisema wakati alipozungumza na wazee wa wilaya za Kibiti na Rufiji, kuwa wanaoendesha mauaji hayo watalipwa ubaya kama wao wanavyofanya.

IGP Sirro alisema daima hali ya mtu mtenda maovu ni kulipwa maovu, hivyo wauaji hao watapatikana na malipo yao yatafanyika ndani ya muda mfupi.

“Pelekeni salamu kwa wauaji hao kwamba ubaya huwa hauwi ubaya siku zote,” alisema.

Wilaya tatu za mkoani Pwani; Kibiti, Rufiji na Mkuranga zimekuwa zikikumbwa na mauaji ya viongozi wa vijiji, watendaji na polisi tangu Mei mwaka jana.

Hali ilionekana kuwa mbaya baada ya watu hao wasiojulikana kulishambulia kwa risasi gari la doria la Jeshi la Polisi na kuua askari tisa waliokuwa wakirejea kutoka zamu.

Askari wengine ambao ni maofisa, waliuawa katika mazingira tofauti; mmoja, Peter Kuponezya aliuawa wakati alipofika eneo ambalo watu hao waliteka kituo cha Idara ya Maliasili na kuagiza wananchi wachukue mali zilizokuwa zimekamatwa na wafanyakazi wa idara hiyo ambao pia baadaye waliuawa, na mwingine, Peter Kubezya aliuawa wakati kikosi cha polisi kilipokwenda kujaribu kukamata watuhumiwa wa uhalifu kwenye nyumba yao iliyo Vikindu.

Viongozi wa vijiji na watendaji wamekuwa wakiuawa kwa kushambulia kwa risasi baada ya kufuatwa na wauaji majumbani kwao nyakati za usiku au mashambani.

Wizara ya Mambo ya Ndani imependekeza kuundwa kwa kanda maalumu itakayoshughulikia wilaya hizo kujaribu kukabiliana na mauaji hayo.

Source: Mwananchi