Mavugo awatuliza Simba kwa staili hii

LAUDIT MAVUGO.

WAKATI uongozi wa Simba SC ukijiandaa kumpokea mshambuliaji wake wa zamani Mganda Emmanuel Okwi, straika wa kimataifa wa timu hiyo kutoka Burundi, Laudit Mavugo, amekanusha taarifa za kujiunga na AS Kigali ya Rwanda.

Akizungumza na gazeti hili kutoka Bujumbura jana, Mavugo, alisema kuwa yeye bado ni mchezaji halali wa Simba na hawezi kusaini mkataba na klabu nyingine kama ilivyoandikwa.

Mavugo alisema kwa sasa anaendelea na mapumziko huku pia akifanya mazoezi mepesi kwa ajili ya kuuweka mwili tayari na maandalizi ya msimu mpya.
"Taarifa hizo si za kweli, mimi bado nina mkataba wa mwaka mmoja na Simba," alisema Mavugo.

Aliongeza kuwa anaamini msimu ujao kwake utakuwa mzuri zaidi kutokana na kuizoea Ligi Kuu na vile vile klabu kusajili wachezaji wengine wapya ambao wana uzoefu na ligi hiyo na mashindano ya kimataifa.

Naye rafiki wa mchezaji huyo, Yusuph Ndikumana anayeichezea Mbao FC alisema kuwa Mavugo hajasaini mkataba na timu nyingine.

"Mavugo ni mchezaji wa Simba, anasubiri likizo imalizike aweze kurudi Tanzania kuendelea na maandalizi ya msimu mpya," alisema Ndikumana.

Okwi ambaye sasa anaichezea SC Villa anatarajiwa kutua nchini kumalizana na uongozi wa Simba baada ya kukubali kusaini mkataba wa miaka miwili.

Simba imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa lengo la kufanya vizuri katika msimu ujao wa ligi na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo watashiriki.

Baadhi ya sura mpya zinazotarajiwa kuvaa jezi ya Wekundu wa Msimbazi katika msimu ujao ni pamoja na John Bocco, Shomari Kapombe, Jamal Mwambeleko, Yusuph Mlipili, Ally Shomary, Aishi Manula na Haruna Niyonzima.