Ajali ya helikopta yakatili maisha ya walinda amani wawili Mali

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, amesikitishwa na taarifa za kuanguka kwa helikopta Jumatano karibu na Tabankort, eneo la Gao Kaskazini mwa Mali.

Kwa mujibu wa taarifa, ajali hiyo iliyosababisha vifo vya walinda amani wawili kutoka Ujerumani ilitokea wakati wakifanya upelelezi Tabankort kufuatia mashambulizi kati ya vikundi viwili vilivyojihami yaliyozuka Julai 11 Kaskazini mwa Mali.

Bwana Lacroix ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa hizo na ametuma salamu za rambirambi kwa familia, jamaa za wahanga ,serikali ya Ujerumani na wafanyakazi wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA.

Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari Jumatano, Naibu msemaji wa Umoja wa Matiafa Farhan Haq amesema

"Kufikia sasa tunaendelea kupokea taarifa kutoka kwa MINUSMA, kwa mfano kilichosababisha ajali na mambo mengine, changamoto ni kwamba helikopta ilikuwa inafanya upelelezi wa mzozo na hivyo eneo hilo limehitajika kuzingirwa kabla ya uchunguzi kuanza."