Watumishi wa afya ambao hawasimamii kikamilifu sera ya matibabu bure kukiona

Serikali imesema itaendelea kuwawajibisha watumishi wa sekta ya afya ambao hawasimamii kikamilifu sera ya matibabu bure kwa kina mama wajawazito na wazee huku wakurugenzi wote wa halmashauri nchini wakiagizwa kuwatambua wazee wasio na uwezo na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bure.

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua utoaji wa vitambulisho vya kutolea huduma za afya bure kwa wazee zaidi ya 3000 wa wilaya ya Kigamboni ambapo amekiri kuwa wazee wamekuwa wakizungushwazungushwa wanapokuwa wanahitaji barua kutoka serikali za mitaa kwa ajili ya kwenda kupata matibabu.

Akizungumza katika uzinduzi huo mkuu wa wilaya ya Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa amesema wanakabiliwa na upungufu wa vituo vya afya ambapo wana hospitali moja tu na vituo vya afya viwili ambavyo havilingani na idadi ya wakazi wa wilaya hiyo, huku mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni Bw. Stephen Katemba akielezea idadi ya wazee waliopo ambao ni zaidi ya elfu saba lakini kwa sasa wameweza kuwatambua elfu tatu tu.