Zitto Kabwe kusomesha wanafunzi 541 bure


Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama Cha ACT Wazalendo, Mhe Zitto Kabwe amefunguka na kusema katika mwaka wa masomo 2017/2018 manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo ipo chini ya chama chake inawasomesha bure jumla ya wanafunzi 541 wa kidato cha tano na cha sita katika shule mbalimbali.

Zitto Kabwe amesema hayo alipozungumza na EATV na kudai kuwa Manispaa ya Kigoma Ujiji imeamua kuwa mfano, kwani ni Manispaa ya kwanza Tanzania kusomesha wanafunzi wake wote wanaomaliza kidato cha nne katika shule zilizopo ndani ya manispaa hiyo na kuwalipia ada katika Elimu ya Juu ya Sekondari
"Tunasomesha bure wanafunzi waliomaliza kidato cha nne katika shule zilizopo ndani ya manispaa yetu ambao wanakwenda popote pale ambapo wanapangiwa kwenda kusoma, mpaka sasa tunasomesha wanafunzi 541, wanafunzi 254 wapo kidato cha tano  na wanafunzi wengine 287 wapo kidato cha sita katika shule mbalimbali, hawa wote wametoka katika shule za manispaa yetu" alisema Zitto Kabwe

Aidha Zitto Kabwe amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji ina mpango wa kuongeza wanasayansi walio wengi hivyo sasa imeamua kujenga shule nyingine ya kidato cha tano na sita ambayo itakuwa ni maalum kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi tu.

"Wakati tunachaguliwa hapa Kigoma shule ya sekondari ya masomo ya juu ilikuwa Kigoma sekondari tu lakini chini ya miaka miwili ambayo tumecahguliwa tayari tumeongeza shule mbili za masomo ya juu yaani kidato cha tano na sita. Sasa hivi tumeamua kuongeza shule nyingine moja ya kidato cha tano na sita ambayo itakuwa ni ya masomo ya sayansi peke yake, tumeamua kufanya hivi sababu tunahitaji wana sayansi zaidi katika mji wetu, tunahitaji vijana wetu wasome sanyansi zaidi" alisisitiza Zitto Kabwe

Manispaa ya Kigoma Ujiji imekuwa manispaa ya kwanza nchini Tanzania kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ambao wametoka katika shule zilizopo ndani ya manispaa hiyo na kwenda shule zingine mbalimbali nchini.