Sumaye afunguka ya Moyoni

Waziri Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Mh. Fredrick Sumaye amedai endapo serikali ingekuwa inawajibika ipasavyo, matukio ya kiuhalifu yasingekuwa yanaendelea kujitokeza mara kwa mara nchini.

Mhe. Sumaye ameeleza kupitia mkutano wa chama hicho na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo ikiwa imepita siku moja tokea kwa tukio lililompata Mhe. Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma 'Area D' na watu wasiofahamika.

"Katika serikali yeyote ambayo inawajibika ipasavyo kazi ya kwanza ya serikiali ni kulinda uhai wa wananchi wake, hiyo ndiyo kazi ya msingi ya serikali. Kwa hiyo kama ni serikali inayowajibika ipasavyo, basi haya matukio yanayoendelea kutokea yasingekuwepo kabisa au basi tukio linapotokea wahusika wangekuwa wanakamatwa kwa haraka na kupelekwa sehemu husika lakini unapokuwa huoni hatua zinazoridhisha zikichukuliwa basi kuna ulakini katika nchi", amesema Sumaye.

Pamoja na hayo, Sumaye ameendelea kwa kusema "kwa sababu serikali ni yetu sote bila ya kujali itikadi ya chama husika. Kwa hiyo mimi nasema kama kweli serikali inawajibika inavyotakiwa basi haya mambo yote ambayo yanatokea yalitakiwa yapatikane majibu ya uhakika na kwani yanapoachwa baadhi ya maeneo yapo gizani basi wengi tunaanza kufikili kwamba utawala unaowajibika unakosekana ama kwa makusudi au kwa uwezo".

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti  wa chama hicho Prof. Abdallah Safari amesema kabla ya Mhe. Tundu Lissu kupigwa risasi alikuwa mtu mwenye wasiwasi mkubwa juu ya maisha yake kutokana na baadhi ya watu waliokuwa wanamfuatilia kwa ukaribu kila kukicha.

"Kabla ya tukio hili kutokea Mhe. Lissu alishawahi kusema katika mkutano wake na waandishi wa habari alikuwa na hofu na maisha yake kutokana na kufuatiliwa na watu wenye gari aina ya Nissan Premier yenye namba za usajili T460 CQV hapa hapa Dar es Salaam. Kwa hiyo maisha ya Lissu yamekuwa yapo hatari kwa kipindi kirefu", amesema Prof. Safari.

Kwa upande mwingine, Prof. Safari amevitaka vyombo vya usalama vitekeleze kazi zake kwa uweledi kama ambavyo wanaweza kufanya katika matukio mengine ya kiuhalifu.