RC Tabora akabidhi Milioni 202 kwa wajasiriamali Kaliua

JUMLA ya shilingi milioni 202 zimetolewa kwa vikundi 89 na Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ikiwa ni sehemu ya mikopo ya kuwezesha vijana , wanawake na walemavu. Fedha hizo zimekabidhiwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa sherehe fupi ya uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake na kukabidhi mkopo iliyofanyika mjini Kaliua na kuhudhuria  na wabunge wa majimbo yote mawili ya Wilaya hiyo.

Alisema mkopo huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa juu ya kutaka kila Halmashauri itenge asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya uwezeshaji wa vikundi vya wanawake asilimia nne, uwezeshaji vijana asilimia nne na uwezeshaji watu wenye ulemavu asilimia mbili.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alitoa wito kwa vikundi vya wanawake vilivyofanikiwa kupata fedha hizo kuzitumia katika malengo waliyoweka ili waweze kuzirejesha kwa ajili ya kuwakopesha wengine. Alisema kuwa ni vema fedha walizokopeshwa wakazitumia kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo na kisha wazirudishe  ili kije kigezo cha siku nyingine kuweza kukopesheka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama aliwakumbusha vikundi vilivyokeshwa kutambua kuwa fedha hizo sio hisani bali ni mkopo ambao wanapaswa kuufanyia kazi ili waweze kupiga hatua na kisha waurejeshe ili vijana na wanawake wenzao nao wapate fursa ya kukopa.

Alisema kuwa wanaimani kuwa kundi hilo likitumia vizuri mikopo hiyo jamii yote ya wilaya itakuwa na maendeleo na uchumi wa Wilaya hiyo utaimarika.
Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kaliua John Pima alisema kuwa wataendelea kuhakikisha kuwa kila mwezi wanatenga fedha kutokana na mapato ya ndani ili baadae wawakopeshe wanawake, vijana na walemavu kwa ajili ya kusaidia kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka.

Naye Mbunge Jimbo la Ulyankulu John Kadutu alitoa wito kwa wakazi wa Wilaya ya Kaliua kuungana katika shughuli za maendeleo bila kujali tofauti za itikadi zao za vyama.
Alisema kuwa yeye na mbunge wa Kaliua ambaye anatoka Chama cha waananchi CUF wamekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wananchi wote na kuwataka viongozi vingine waige mfano huo.

Wakati huo huo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imetoa pikipiki nane zenye thamani ya shilingi milioni 18.9 kwa ajili ya Maafisa Ugani wanne na Watendaji wa Kata wanne ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wakazi wa maneo yao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Pima , pikipiki hizo zinalenga kuwaondolewa Maafisa Ugani uhaba wa usafiri ili waweze kuwahudumia vizuri wakulima na kuwasaidia ili waweze kupata mazao mengi na bora. Alisema kuwa wakati mwingine ilikuwa vigumu kwa Maafisa Ugani kuwafikia wakulima kwa sababu ya kuwa mbali na hivyo vyombo hivyo wa usafiri vitasaidia kuondoa visingizio kwa watumishi hao.

Kuhusu watendaji wa Kata kupata usafiri huo alisema kuwa zitawasaidia kuimarisha shughuli za utawala ikiwemo kusikiliza kero na matatizo mbalimbali ya wananchi na kuwaondolea shida ya wananchi  kusafiri umbali mrefu ili kuwafuata viongozi. Akiongea wakati wa kukabidhi pikipiki hizo kwa watumishi hao Mkuu wa Mkoa wa Tabora aliwaonya kutumia vyombo hivyo kuwasaidia wananchi na sio kwa maslahi binafsia kama vile kubeba mizigo na wakati mwingine kuzigeuza bodaboda.

Alisema kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua kali ili ije iwe fundisho kwa wengine. Watendaji walipata pikipiki wanatoka kata za Ilege, Igwisi, Usimba na Nhwande na kwa upande wa Maafisa Ugani watoka kata za Seleli, Zugumlole, Silambo na Ukimbisiganga.