Samatta azidi kuiokoa KRC Genk

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa jana ametoa pasi iliyoipa bao la kusawazisha KRC Genk ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Royal Excel Mouscron nyumbani katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.

Samatta usiku wa jana alicheza kwa dakika zote 90 timu yake, KRC Genk ikiendelea kupita katika msimu mbaya kwa kunusurika kufungwa nyumbani.

Na jana, Samatta hakuwa na bahati ya kufunga tu, lakini alipambana mno kwa muda wote wa mchezo, akicheza bila kuchoka, lakini bahati haikuwa yake. 

Pamoja na hayo, Samatta akamsetia Marcus Ingvartsen kuifungia Genk bao la kusawazisha dakika ya 81, baada ya wageni kutangulia kwa bao la Dorin Rotariu aliyeimalizia pasi ya Sebastien Locigno dakika ya 42.

Hiyo inakuwa mechi ya 66 kwa Samatta Genk katika mashindano yote tangu Januari mwaka jana alipojiunga na timu hiyo akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika mechi hizo, Samatta ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka jana alipokuwa na Mazembe, 38 ameanza na mechi 24 ametokea benchi.

Katika mechi hizo, mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon, zamani Mbagala Market na Simba zote za Dar es Salaam, amefunga jumla ya mabao 21 kwenye mashindano yote.

Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa; Vukovic, Mata, Aidoo, Colley, Uronen/Khammas dk78, Berge, Malinovskyi, Pozuelo/Buffalo dk73, Writers/Benson dk64, Samatta na Ingvartsen.

RE Mouscron : Bailly, Govea, Olinga/Vojvoda dk63, Aidara/Boya dk82, Mohamed, Awoniyi/Mbombo dk85, Locigno, Diedhiou, Nkaka, Huyghebaert na Rotariu.