Baada ya Tambwe kurudi uwanjani, mabadiliko yafanyika

Mshambuliaji wa Yanga Mrundi, Amissi Tambwe.

KUREJEA kwa mshambuliaji wa Yanga Mrundi, Amissi Tambwe kumekifumua kikosi cha Mzambia, George Lwandamina ambaye atalazimika kumuondoa mchezaji mmoja katika ‘first eleven’.

Tambwe anarejea uwanjani akitokea kwenye majeraha ya goti yaliyomsababisha kuzikosa mechi zote za Ligi Kuu Bara ambazo timu yake imezicheza tangu ligi hiyo imeanza msimu huu.

Mshambuliaji huyo, kesho Jumamosi huenda akawepo kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachoivaa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Azam Complex uliokuwepo, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Lwandamina alionekana kufanya mabadiliko hayo katika mazoezi ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar baada ya kupanga vikosi viwili na kucheza mechi mazoezi.

Katika kikosi chake cha kwanza, aliwapanga wachezaji watakaoanza katika kikosi cha kwanza huku akimpanga Tambwe katika kikosi cha pili cha akiba.

Kikosi cha kwanza kilipangwa kama ifuatavyo kipa; Rostand Youthe, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Pato Ngonyani, Pius Buswita, Raphael Daudi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.

Wakati mazoezi hayo yanaendelea, katika kipindi cha pili alifanya mabadiliko kwa kumtoa Martin katika kikosi cha kwanza na kumuingiza Tambwe aliyekuwepo katika kikosi cha pili.

Lwandamina mara baada ya kufanya mabadiliko hayo, alimpeleka Ajibu katika nafasi ya Martin aliyokuwa anaicheza ambayo ni namba 11 na Tambwe kucheza 10 aliyokuwa anaicheza Ajibu.

Lengo la kuwapanga Tambwe na Chirwa ni kuwachezesha washambuliaji wawili wenye uwezo wa kufunga mabao ili timu yake ifunge mabao mengi kwenye mechi zijazo ikiwemo dhidi ya Prisons.

Mara baada ya mazoezi hayo, Tambwe alizungumza na Championi Ijumaa na kusema: “Ninafurahi kurejea uwanjani nikiwa fiti kabisa, ukweli nilimisi kucheza lakini majeraha ndiyo yalinizuia.”